Kasa: Mnyama mpole mwenye maajabu mengi

By Nasibu Mahinya

  • Hutambulika kama kobe wa majini.
  • Anaishi majini, anatotolesha mayai ufukweni.

Karibu kila mnyama wa ardhini ana ndugu yake wa majini ambaye hufanana naye kimuonekano na hata tabia wakati mwingine.

Ukiona kobe anaogelea basi jua mapema kuwa huyo siyo kobe, huyo ni kasa.

Kasa ni mnyama wa majini ambaye wengi humfananisha na kobe kwa sababu ya ufanano wao wa zaidi ya asilimia 90.

Kasa ni mnyama mkongwe ambaye anasemekana kuwepo duniani kwa zaidi ya miaka millioni mia.

Wengi wamekuwa wakimuita â€˜kobe wa majini’ au â€˜kobe maji’ na inajulikana hivyo lakini hawa ni wanyama wawili tofauti na leo nitakupa sifa tisa za kasa ili tuweze kumjua zaidi kiumbe huyu.

1. Kasa ni mnyama wa majini ambaye hutaga mayai yake ardhini na ana tabia ya kuyafukia mayai yake kwa mchanga ufukweni.

2. Kasa hujamiiana kipindi cha miezi ya Machi mpaka Oktoba yani mwezi wa tatu hadi wa kumi.

3. Kasa huja nchi kavu kutaga mayai na kuyafukia tu na kisha kuondoka bila kurudi tena. Hutaga zaidi

ya mayai sabini ambayo hutotoa ndani ya siku sitini.

4. Mayai ya kasa hutotoa yakiwa yamefukiwa na mchanga hivyo kumlazimisha kinda wa kasa kufukua na kuibuka kutoka mchangani na kuanza kuelekea majini.

5. Jinsia ya kasa anayetotolewa hutegemea na joto la mchanga. Zikizidi nyuzi joto 30° basi yai hutotoa jike na zinapopungua nyuzi joto 30° basi yai hutotoa dume. Uzao wa makasa jike umekuwa ukiathiriwa katika maeneo  yanayokumbwa na majanga ya tabianchi, hivyo kusababisha ongezeko la joto na matokeo yake ni upungufu wa makasa jike na kuathiri uzao wao kwa ujumla. 

6. Mara nyingi kasa jike hurudi kutaga mayai pale alipototolewa yeye. Kama kabila flani wanavyorudi kwao kila ifikapo Krismasi hahahah! Natania.

7. Idadi kamili ya kasa waliopo duniani haijulikani kwa sababu kasa dume huwa hawarudi tena nchi kavu baada ya kutotolewa hivyo ni ngumu kuwahesabu.

8. Kasa anaweza kuwa na uzito wa hadi kilo 900 na anaweza kuishi mpaka miaka 80.

9. Tofauti na alivyo kobe, kasa hawezi kuingia ndani ya jumba lake, hivyo kichwa na miguu yake hubaki nje ya gamba muda wote.

Kasa wanapatikana kwa wingi visiwani Zanzibar na Mafia. Unaweza kucheza nao na kuogelea nao kwenye bwawa maalum au baharini chini ya maji. 

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Scroll to Top