AFYA ni nini?

By Maureen C. Minanago Afya ni hali ya kutokuwa na ugonjwa au kidonda. Afya ni hali ya kuwa na amani ya roho. Afya ni ubora wa akili, mwili na nafsi. Afya hutegemea vitu hivi vitatu ili kuwa hai na salama: Akili, Mwili, Nafsi. Akili ni utashi tuliopewa na Mwenyezi Mungu katika kung’amua mambo ulimwenguni. Akili hujumuisha uelewa, ufikiri, uamuzi na utendaji wa mambo. Hakuna awezaye kutafsiri akili yetu ila matendo yetu yanaweza kumfanya mtu aone flani yuko vipi; nayo bado itakuwa mtazamo wake sababu tunatofautiana kufikiri pia.  Binadamu hutumia akili kila siku na kila wakati ili kuelewa, kufikiri, kuamua na kuhakikisha tunatimiza jambo. Kwa maana hiyo, tunapaswa kuipumzisha “PUMZISHA AKILI”. Akili ikichoka mwili nao huchoka na hutafanya chochote sababu haitakuwa na uwezo mzuri kutenda. Lala au oga au ogelea au sikiliza mziki au chochote ukipendacho ambacho hakitakufanya utumie nguvu ya akili. Mwili ni muundo wote wa binaadam. Ni maumbile ya mtu. Mwili huhusisha yote yaliyotengeneza “mtu” mfano viungo kama miguu, mikono n.k, Maji kama mate, damu n.k, na vingine kama mishipa kucha na nywele. Tunapaswa kujipenda kwa kula vizuri, kulala vizuri na pazuri, kuvaa vizuri na kujijali muda wote kwa kuuweka mwili salama mfano kwa kupiga mswaki baada ya kula, kuosha nywele mara kwa mara, kukata na kusafisha kucha, kuoga, na kuvaa nguo safi. Pia tujiepushe na hatari, ugomvi na makwazo kwa faida ya mioyo yetu.  Ukitembea sana juani pata kivuli unywe na maji. Penye baridi uvike mwili wako kwa sweta ama nguo nzito. Ukiumia au kuumwa pata matibabu sahihi kwa kwenda hospitalini. Jipende, Ujali mwili wako. Tukifanya hivyo miili yetu itakuwa salama.  Nafsi ni roho yenye kuleta imani ndani yetu. Sisi huamini vitu mbali mbali kwa msaada wa nafsi. Lakini yote heri kama tutaamini vitu vyenye kujenga na sio kubomoa. Nafsi pia hutofautiana ya mtu na mwingine ndio maana tukawa tofauti japo chimbuko letu kiuumbaji ni moja.  Nafsi nayo huhitaji utulivu ili kuupa mwili na akili nguvu za kuishi kwa afya. Pata muda wa kutulia ukiongea na WEWE kujua nini waweza fanya LAKINI, mshirikishe MUUMBA wako kwa yote kupata amani uitakayo moyoni na kwa wakuzungukao. Hivyo basi, jipe likizo au omba likizo. Tembelea sehemu mbali mbali za starehe au vivutio kutuliza mwili, akili na roho pia. Ongea vizuri na watu, cheka, tabasamu hata kama umeumizwa. Inasaidia sana.  Afya ya vitu vyote vitatu ni muhimu katika kukuweka mwenye nguvu na furaha.  Jali afya yako!

AFYA ni nini? Read Post »

Moyo wa Binadamu

By Maureen C. Minanago Je, unaufahamu kuwa kila mwanadamu anapumua kwa msaada wa moyo? Na je, unafahamu kuwa moyo huo huo unaweza kumfanya mtu kuwa na furaha ama huzuni? Hii ni alama ambayo wengi huitumia kuashiria moyo na moyo huo basi unatumika kama ishara ya upendo. Moyo ni pampu inayosukuma damu kupitia mishipa ya damu. Kupitia mishipa hiyo damu husambazwa mwili mzima ili kukupatia hewa safi (oxygen). Tukiachana na maswala ya kibaiolojia, moyo unakazi ya kupenda. Basi tuone upendo huo unaathiri vipi moyo na wewe kama binadamu unaukosea vipi moyo wako ama moyo wa mwingine. Jijali, mjali na mwenzio ili kuufurahisha moyo kwa afya zaidi. Huu ni moyo wa binadamu. Unapokuwa umezungukwa na watu wakupendao haijalishi ni upendo wa aina gani, moyo huwa na nguvu na hufanya kazi yake vizuri. Kila mmoja anapenda kupendwa, hata wababe huwa na wafuasi wao hata kama hawana upendo wa dhati. Moyo wenye furaha. Moyo wenye nguvu… Moyo wenye furaha huimba ndani yetu pale tunapoongeza marafiki wapya. Moyo wenye furaha huupoza mwili tusikiapo baridi yaani tuwapo wapweke, kwa kukumbuka mema mengi yaliyopita. Inawezekana kabisa kwa wewe kujichangamsha bila kusubiri kuchangamshwa. Moyo imara ni moyo wenye nguvu kwani unaweza kupigana na majaribu yote yanayotukumba katika maisha. Sisi sote tunapaswa kuwa na moyo wenye nguvu kwani pia ni rahisi kupingana na magonjwa tukianza na ugonjwa wa ‘moyo’ wenyewe. Upendo wa nguvu Upendo wa mahusiano ya kimapenzi ni upendo unaoleta hisia za kipekee. Kila mmoja anaweza kuuelezea ajuavyo yeye. LAKINI, maumivu ya kuachana kwa wapenzi hao yanaweza kuwa yanafanana kwani yote huumiza moyo. Upendo unaolega lega Afya ya mtu ni ya thamani, ni vema kutumia nafasi unayopata kwa mpenzi wako kumuonesha upendo na kupata upendo kutoka kwake. Kama unadhani hujaamua bado kujiingiza kwenye mahusiano, basi tafakari kabla ya kuchukua hatua. Ni vema kujiamini kwa ulifanyalo kuepukana na maumivu ya moyo. Kipindi tu unapojihusisha na mahusiano ya kimapenzi, fahamu kuwa unajifunga. Moyo uliofungwa kwa upendaye, usiufungulie kwa wengine. Angalizo: Ili kuulinda moyo (wako/mwemzako) na maumivu zingatia haya:- Ukipata mwenzako mshikilie sawa sawa. Ni bora kuumia kidole kitapona au kuvunjika kidole vingine vitafanya kazi lakini sio kuumia moyo sababu maumivu yake yaweza kuchukua miaka kuisha na kuvunjika kwa moyo ni ngumu kuutengeneza ukafanya kazi sawia. Kuna Moyo usioweza kufanya maamuzi sahihi, Moyo ulionyong’onyea na kudhoofika na Moyo uliochanganyikiwa. Hapa ndipo tunaposhauriwa kuwa na imani kwa kumuomba Mungu kwani yeye ndiye aliyekupa maisha. Jijali kwa kuepukana na athari hizo lakini pia, kama ikitokea ushaumizwa basi jitahidi kujishughulisha sana ili kupunguza mawazo. Kaa na watu watakupa mawazo tofauti usikae mwenyewe ukiwa mpweke kuepukana na mawazo potofu. Kemea roho ndani yako inayokusukuma kukata tamaa, kuchukia ama kujiua. Sali sana ukisikia hivyo kwa afya ya Roho na moyo pia. Maumivu makali ya moyo Usiuzeeshe moyo wako kwa mambo usiyoyaweza. Usiukondeshe kwa kuupa mambo mengi usiyoweza kuyafuatilia na kuyafanya kwa ufanisi, usiufanye ukaelemewa. Ujali moyo wako kwa kujipenda na kuwa makini. Lakini kikubwa, usiutegemee moyo pekee katika mapenzi, shirikisha akili yako. Ni kwa kufanya hivyo, moyo utabaki kupenda tu huku mengine yakifanywa kwa utashi uliobarikiwa nao.

Moyo wa Binadamu Read Post »

Wewe ni wa Thamani

By Maureen C. Minanago Wewe ni wa Thamani!!! Jifunze umuhimu wako wewe kama binadamu kama utazingatia afya bora kwako na kwa mwenzako. Kula chakula chenye lishe na kufanya mazoezi ni changamoto kwa wengi hasa ukizingatia mfumo wa maisha kwa wengi hivi sasa. Lakini, ni afya njema tu itakayokupa nguvu ya kufanya yaliyo mazito na wepesi wa kufanya yaliyo magumu. Lishe inayoenda na mazoezi kiasi itakuepusha wewe na magonjwa kama kisukari, presha ya damu, unene wa kupindukia, kansa na mtindio wa ubongo. Badala yake hukupa vitu kama upeo mzuri wa kufikiri, nguvu, amani, wepesi, mzunguko mzuri wa damu na wa chakula, kwa kutaja machache. Mstari mmoja wa kitabu cha dini unasema “Watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa”. Usijiachie ukasahau kutunza afya yako kwani wewe ni wa muhimu sana katika ulimwengu huu. Mungu hakukosea kukuumba hivyo ishi kwa kujali afya yako ili uwe na maisha yenye furaha. Magonjwa hututoa furaha, unene hutunyima uhuru kufanya baadhi ya vitu, kwa nini basi tusijitunze kwa kuzingatia lishe na mazoezi ili kupata afya na nguvu tele?! Usiwe nyuma katika kujua afya yako, pima mara kwa mara na ufanye tafiti hasa kwa kusoma nyaraka mbali mbali za afya ili uwe kwenye njia sahihi.

Wewe ni wa Thamani Read Post »

Scroll to Top