ONGEZEKO LA WATOTO WA MITAANI  

By Jamal H. Maherea Nanukuhu kutoka tovuti ya Jamii Forum 2022, “Watoto wa mitaani, ni watoto ambao wanaishi mitaani, nje ya makazi ya kawaida. Kempe Ronald Hope, (2005) anatoa maana ya Mtoto wa Mitaani kama ifuatavyo: “Mtoto wa Mtaani, ni msichana au mvulana ambaye hajafikia umri wa utu uzima, ambapo mtaa (ikijumuisha makazi yasiyokaliwa, maeneo yenye mazingira magumu, na kadhalika) umekuwa makazi, na mahali pa kujikimu kimaisha, ambaye hana ulinzi wa kutosha na ambaye haongozwi na watu wazima wenye kuwajibika”. Ongezeko la watoto wa mitaani ni changamoto kubwa inayowakumba watoto wengi ulimwenguni ikiwemo Tanzania. watoto hawa, ambao wanakosa makazi salama na malezi ya wazazi au walezi, hukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoathiri maisha yao ya kila siku. Watoto wa mitaani ni wale wanaoishi na kufanya kazi katika mazingira hatarishi ya mtaani, hali inayowafanya kuwa katika hatari ya kukosa elimu, afya bora, na fursa ya kujitengenezea maisha yenye mafanikio. Makala hii itachambua sababu zinazochangia ongezeko la watoto wa mitaani nchini Tanzania, athari wanazokabiliana nazo, na kutoa mapendekezo ya namna ya kuwasaidia watoto hawa. SABABU ZA ONGEZEKO LA WATOTO WA MITAANI UMASKINI Umaskini ndio chanzo kikuu cha watoto wengi kujikuta mitaani. Familia maskini hushindwa kumudu mahitaji ya msingi ya watoto kama chakula, mavazi, na elimu. Hali hii huwalazimisha watoto kutafuta njia za kujikimu mitaani. Watoto kutoka familia maskini katika mikoa mbalimbali ikiwemo Singida hukimbilia kwenye miji mikubwa kama Dar es Salaam na Mwanza kwa matumaini ya kupata kipato. Kwa mujibu wa Mama Lily ambaye ni mama mlezi wa kituo cha KINDAI SAFINA Singida, anaeleza baadhi ya watoto waliopo katika kituo hicho cha malezi ni kutokana na changamoto ya umaskini uliopo katika familia zao. Umaskini huo, huwapelekea watoto kutoka katika familia hizo kuanza kuzurura mitaani na wengine kujiingiza katika tabia zisizofaa. MIGOGORO YA KIFAMILIA VIFO VYA WAZAZI    Migogoro ya kifamilia, kama vile talaka na ugomvi wa wazazi, huathiri watoto kisaikolojia na mara nyingine kuwaacha bila malezi. Watoto wanaopitia changamoto hizi hukimbilia mitaani kutafuta uhuru au kujitafutia riziki. Kwa mfano, baadhi ya watoto wanaoishi mitaani katika miji ya Dodoma na Singida wamekimbia migogoro ndani ya familia zao. Vifo vya wazazi kutokana na magonjwa kama ukimwi au ajali vimeacha watoto wengi kama yatima, ambao hawana uangalizi wa kifamilia. Watoto hawa, hasa katika mikoa kama Dodoma na Singida, hukosa msaada wa kifedha na kimaadili, na hivyo kulazimika kujikimu mitaani.  Kupitia kituo cha KINDAI SAFINA Singida pamoja na SAVE THE CHILD kilichopo Dodoma wanaeleza kuwa baadhi ya Watoto hukimbia nyumba kutokana na migogoro ya familia inayowajengea uwonga na kuwapelekea kujiingiza katika kundi la Watoto wa mitaani. ATHARI ZA KUISHI MITAANI KWA WATOTO KUKOSA ELIMU NA AFYA BORA Watoto wa mitaani mara nyingi hukosa fursa ya kupata elimu ya msingi na sekondari kutokana na kutokuwa na msaada wa kifedha au wa kifamilia. Hali hii huzuia maendeleo yao ya kitaaluma na kuwapunguzia nafasi za kujiendeleza kiuchumi hapo baadaye. Watoto wa mitaani hukosa lishe bora, malazi salama, na huduma za afya za msingi. Hii inawaweka katika hatari ya kupata magonjwa kama vile utapiamlo, malaria, na maambukizi ya njia ya hewa. Pia, wengi wao hujiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya na pombe kwa sababu ya mazingira wanayoishi, hali inayozidi kuathiri afya zao. Kupitia kituo cha KINDAI SAFINA Singida Mama Lily amelithibitisha hili kwa kuwa na baadhi ya watoto ambao walikuwa hawafahamu kusoma na kuandika. KUHARIBIKA KISAIKOLOJIA KUINGIA KWENYE MAKUNDI HATARI Maisha ya mitaani huathiri afya ya akili ya watoto, na wengi wao hukumbana na msongo wa mawazo na kiwewe kutokana na changamoto wanazopitia kama unyanyasaji, upweke, na kukataliwa na jamii. Watoto wa mitaani wanapokuwa bila mwongozo wa kifamilia wanaweza kujiunga na makundi ya kihalifu, na kujiingiza kwenye uhalifu mdogo au kuathiriwa na magenge yanayohusishwa na vitendo vya uhalifu. Mfano halisi, mkoa wa Singida unakumbwa na tatizo hili la ongezeko la watoto wa mitaa ambao wengi huuishia kuvuta gundi, bangi na uwizi. Baadhi ya wafanyabiashara katika soko kuu la Singida, wanalalamikia sana watu wanaofanya biashara ya kuwauzia gundi baadhi ya watoto wa mitaani. Hali hii inawaweka katika hatari ya kukamatwa na polisi au kujiingiza kwenye mizozo hatarishi. NAMNA YA KUWASAIDIA WATOTO WA MITAANI KUWEZESHA FAMILIA MASKINI KUPITIA MISAADA YA KIFEDHA Misaada ya kifedha kwa familia maskini inaweza kusaidia kupunguza tatizo la watoto wa mitaani. Programu kama TASAF (Tanzania Social Action Fund) zinatoa misaada kwa familia maskini ili kuimarisha hali zao za maisha na kupunguza watoto kutoroka nyumbani. Kupitia misaada ya kifedha, familia zenye hali duni zitaweza kujikwamua katika hali duni ya kimaisha na kuwekeza nguvu pia katika uangalizi wa watoto wao. Hii itachangia zaidi katika kupunguza ongezeko la watoto wa mitaani kwa kiasi kikubwa. KUTOA ELIMU NA MAFUNZO YA KUJITEGEMEA Elimu ni nyenzo muhimu ya kumsaidia mtoto kuondokana na umasikini. Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali yanaweza kuanzisha programu za mafunzo ya ufundi stadi kwa watoto wa mitaani, kama vile ushonaji, useremala, na uashi. Hii itawasaidia kupata ujuzi wa kujiajiri na kujitegemea. KAMPENI ZA KUELIMISHA JAMII KUHUSU HAKI ZA WATOTO Kampeni za kuelimisha jamii kuhusu haki za watoto ni muhimu sana katika kuimarisha ustawi wa watoto na kujenga jamii yenye ufahamu wa majukumu yao katika malezi bora. Kampeni hizi zinalenga kutoa elimu juu ya haki za watoto, kuwahamasisha wazazi, walezi, na jamii kwa ujumla kutimiza wajibu wao katika kuwalinda na kuwaendeleza watoto. Jamii inaweza kushiriki katika kampeni za kuelimisha kuhusu haki za watoto, umuhimu wa kuwalea watoto katika mazingira bora, na kusaidia kupunguza unyanyasaji na unyanyapaa dhidi ya watoto wa mitaani. Hivyo, ongezeko la watoto wa mitaani nchini Tanzania ni changamoto inayohitaji jitihada za pamoja kutoka kwa serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, na jamii kwa ujumla. Watoto hawa wanahitaji msaada wa haraka ili kuwapa nafasi ya kuishi maisha yenye matumaini na mustakabali mzuri. Kwa kuweka mipango thabiti na programu za kuwasaidia watoto wa mitaani, Tanzania inaweza kupunguza ongezeko hili na kuwasaidia watoto hawa kutimiza ndoto zao na kuchangia katika maendeleo ya taifa.

ONGEZEKO LA WATOTO WA MITAANI   Read Post »

JINSI AKILI INAVYOSAFIRI KUTOKA WAZO MOJA HADI LINGINE

By Sylvia E. Mtenga Akili ya binadamu ni kitu cha kushangaza na chenye uwezo wa ajabu. Ina uwezo wa kusafiri kutoka wazo moja hadi lingine, kukumbuka matukio ya zamani, na hata kuwaza juu ya yajayo. Hii inaitwa “safari ya mawazo,” ambayo inahusisha jinsi akili inavyotembea kutoka fikra moja hadi nyingine kwa haraka, kwa mpangilio fulani au bila mpangilio. Hata hivyo, safari hii ya mawazo mara nyingi hutegemea hisia, mazingira, na hali ya akili ya mtu, na ina uwezo wa kuathiri maisha ya mtu kwa njia mbalimbali. 1. Akili inavyokumbuka yaliyopita. Kumbukumbu ni sehemu muhimu ya safari ya mawazo. Akili inapotaka kukumbuka matukio ya zamani, inasafiri kwenye sehemu mbalimbali za kumbukumbu, ambapo habari tofauti zinazohusiana na tukio hilo huhifadhiwa. Kumbukumbu hizi zimegawanywa katika makundi mawili makubwa: kumbukumbu ya muda mfupi na kumbukumbu ya muda mrefu. Kumbukumbu za muda mfupi zinajumuisha mambo ambayo akili imepokea hivi karibuni, huku kumbukumbu za muda mrefu zikihifadhi mambo muhimu zaidi yanayowezesha akili kurudi kwenye yaliyopita kwa undani. Hii ndiyo sababu tunapokumbuka matukio ya kale, mara nyingi tunaweza pia kukumbuka hisia, hali ya hewa, na mazingira ya wakati huo. Hata hivyo, kumbukumbu za zamani zinaweza pia kutuathiri ikiwa tunazifikiria sana. Kwa mfano, mtu anayekumbuka kwa wingi mambo ya huzuni au majuto ya kale anaweza kukumbwa na msongo wa mawazo au huzuni. Hii ni kwa sababu akili inaelekea kuingiza hisia ya wakati uliopita katika hali ya sasa, na hivyo kuathiri hisia na mtazamo wa mtu kwa wakati huu. 2. Akili inavyowaza yajayo. Kuwaza yajayo ni sehemu muhimu ya safari ya mawazo na huwawezesha binadamu kupanga mipango, kujiwekea malengo, na kuwa na mtazamo wa kuendeleza maisha. Akili inapotafakari yajayo, huchukua matukio yaliyopita kama msingi wa kutabiri na kujiandaa kwa wakati ujao. Hii inahusisha mchakato wa kufikiria matokeo tofauti yanayoweza kutokea, kutathmini uwezekano wa matukio, na kuamua hatua zinazofaa kuchukuliwa ili kufikia malengo yaliyowekwa. Lakini, kama ilivyo kwa kumbukumbu za zamani, kuwaza sana juu ya yajayo kunaweza kuwa na madhara yake. Mtu anayekazia sana mawazo juu ya mustakabali anaweza kuanza kuhisi wasiwasi, hofu, au hata kuwa na tabia za kutojali hali ya sasa. Wasiwasi huu unaweza kumfanya mtu kutokuwa na utulivu wa akili na hata kupoteza furaha ya wakati wa sasa, jambo ambalo linaweza kuathiri ubora wa maisha ya mtu. 3. Athari za kuwaza sana yaliyopita au yajayo. Kama akili inavyotumia kumbukumbu za zamani na mawazo ya yajayo, mara nyingi hutokea kuwa watu hupotea katika mawazo haya kwa kiasi cha kuathiri maisha yao ya sasa. Kuwaza sana yaliyopita au kuwaza sana yajayo kunaweza kusababisha msongo wa mawazo, wasiwasi, na hata hali ya kukosa kujiamini. Athari hizi zinaweza kutokea kwa njia mbalimbali. Wakati akili inapotumia muda mwingi kufikiria matukio ya zamani, inaweza kumfanya mtu kuwa na hali ya kutoridhika na maisha, kujilaumu, au hata kushindwa kusonga mbele. Hii ni kwa sababu mtu anaelekea kuona makosa au mambo aliyoyakosa na kutotilia mkazo mafanikio au mambo mazuri aliyoyapata. Kwa upande mwingine, kuwaza sana juu ya yajayo kunaweza kumfanya mtu kuwa na hali ya wasiwasi wa kila wakati, kwa kuwa akili inahofia mambo yasiyojulikana ambayo yanaweza kutokea. Wasiwasi huu unaweza kupelekea mtu kushindwa kufurahia hali halisi ya sasa na kuishi kwa shinikizo kubwa la maisha.

JINSI AKILI INAVYOSAFIRI KUTOKA WAZO MOJA HADI LINGINE Read Post »

KUJIFUNZA KUACHILIA: NJIA YA KUJIPONYA AKILI NA KUMBUKUMBU MBAYA

By Sylvia Mtenga Katika safari ya maisha, mara nyingi tunakutana na changamoto, maumivu, na kumbukumbu ambazo zinaweza kutuzuia kuishi kwa amani na furaha. Kujifunza kuachilia ni mojawapo ya njia muhimu za kujiponya kiakili na kimaisha. Ni mchakato wa kuuachia mzigo wa hisia hasi, majuto, na hali za zamani ambazo zinaweza kuwa zinatuzuia kufikia hali ya utulivu wa ndani. Katika makala hii, tutachunguza kwa undani maana ya kuachilia, kwa nini ni muhimu, na jinsi unavyoweza kufanikiwa katika mchakato huu wa uponyaji. Maana ya Kujifunza Kuachilia Kujifunza kuachilia kunahusisha kuruhusu hali, hisia, au watu ambao hawana tena nafasi nzuri katika maisha yako kuondoka kwa amani. Inaweza kuwa ni kuachilia hali ngumu uliyoipitia, maumivu ya kihisia, au hata matarajio usiyotimiza. Ni kitendo cha kukubali hali halisi, kujipatanisha na yaliyopita, na kuruhusu nafsi yako kuendelea mbele bila kubeba mzigo wa hisia hasi. Kwa Nini Ni Muhimu Kujifunza Kuachilia? Njia za Kuanza Mchakato wa Kuachilia Kujifunza kuachilia si jambo rahisi, hasa ikiwa hali zinazokukumba ni nzito au zina maumivu makali. Hata hivyo, kwa kutumia njia zifuatazo, unaweza kuanza mchakato huu wa uponyaji wa kina: 1. Kubali Hisia Zako Mchakato wa kuachilia unaanza na kukubali kile unachokihisi. Huwezi kuachilia jambo ambalo hukubali kwamba linakupa maumivu au linakuhuzunisha. Ruhusu nafsi yako ihisi huzuni, hasira, au hofu, lakini usikubali hisia hizo zikufunge. Kukubali hisia ni hatua ya kwanza ya kuelekea uhuru. 2. Jifunze Kujisamehe Mara nyingi tunakuwa wagumu kujisamehe kutokana na makosa tuliyoyafanya. Kujisamehe ni hatua muhimu ya kuachilia. Unapokubali kuwa binadamu ni kiumbe kisichokamilika, unaanza kujijengea uwezo wa kujiponya na kuendelea mbele. Makosa ni sehemu ya kujifunza; acha makosa yako yawe somo na sio mzigo. 3. Zingatia Kile Unachoweza Kudhibiti Mambo mengi yanayotulemea huwa hayadhibitiwi na sisi. Kujifunza kuachilia kunahusisha kutambua mipaka ya udhibiti wetu. Zingatia kile unachoweza kubadilisha katika hali zako, lakini achilia yale ambayo yako nje ya uwezo wako. Kufanya hivi kutakusaidia kujenga nguvu na utulivu wa akili. 4. Fanya Mazoezi ya Kutafakari na Kuwa Makini (Mindfulness) Kutafakari na mazoezi ya kuwa makini yanasaidia kuzingatia wakati wa sasa na kuachilia mawazo ya zamani au wasiwasi wa baadaye. Kwa njia hii, unajipa nafasi ya kufurahia maisha bila kufungwa na fikra za zamani. Mazoezi ya kupumua kwa kina, yoga, na kutafakari kwa utulivu vinaweza kusaidia akili kutulia na kufungua njia ya kuachilia. 5. Zungumza na Mtu wa Kuamini Kuzungumza kuhusu maumivu yako na mtu unayemwamini kunaweza kuwa njia bora ya kuachilia hisia zinazokusumbua. Watu wa karibu wanaweza kukusaidia kuona hali kwa mtazamo tofauti au hata kutoa msaada wa kihisia. Ushauri wa kitaalamu kutoka kwa mwanasaikolojia au mshauri pia unaweza kusaidia katika safari ya kuachilia. 6. Pata Masomo Kutokana na Changamoto Badala ya kujikamata kwenye maumivu au hali hasi, tafuta masomo kutokana na hali hizo. Je, umejifunza nini kutokana na hali iliyokukumba? Masomo haya yanaweza kukusaidia kuepuka hali kama hiyo tena na pia kukupa nguvu ya kushughulikia changamoto kwa njia bora zaidi siku zijazo. Msomaji, kujifunza kuachilia ni zawadi unayoipa nafsi yako. Ni mchakato wa ukombozi wa ndani unaokuwezesha kuishi maisha yaliyojaa amani, furaha, na utulivu wa akili. Ingawa inaweza kuchukua muda, kwa uvumilivu na kujitolea, unaweza kufanikiwa kuondoa vizuizi vya kihisia vinavyokuzuia. Hatua kwa hatua, utaanza kuhisi uzito unapungua, na akili yako itapata nafasi ya kujiponya. Kumbuka, kuachilia sio ishara ya udhaifu, bali ni ishara ya hekima na ujasiri wa kuendelea mbele.

KUJIFUNZA KUACHILIA: NJIA YA KUJIPONYA AKILI NA KUMBUKUMBU MBAYA Read Post »

KITOVU CHA UTALII TANZANIA

By Jamal H. Maherea Arusha ni mojawapo ya maeneo ya kipekee barani Afrika ambayo yamebarikiwa kuwa na vivutio vya kipekee vya utalii, ikiwemo hifadhi za wanyamapori, milima yenye mandhari nzuri, na tamaduni tajiri za wenyeji. Arusha ni mji unaounganisha urithi wa asili na utajiri wa utamaduni, na hivyo kuifanya kuwa kivutio muhimu kwa wale wanaotafuta uzuri wa asili wa Afrika Mashariki.  Twende kutazamia baadhi ya vivutio vinavyoupamba mji wa Arusha na kuufanya kuwa kitovu cha utalii.  HIFADHI ZA TAIFA Arusha ni kitovu cha safari za kitalii kutokana na ukaribu wake na hifadhi nyingi maarufu za taifa. Moja ya hifadhi maarufu duniani, Serengeti inayojulikana kwa tukio la uhamaji mkubwa wa nyumbu, ambapo nyumbu huenda kutafuta malisho mapya. Ngorongoro Crater ni kivutio cha kipekee ambacho ni volkano kubwa iliyozama na sasa ni makazi ya aina mbalimbali za wanyama, ikiwa ni pamoja na simba, faru weusi, tembo, na pundamilia. Watalii katika hifadhi ya Taifa ya Arusha, wanaweza kufanya safari za miguu (walking safaris), ambayo ni nadra kulinganishwa na hifadhi nyingine. Pia, hifadhi hii ni maarufu kwa nyani, twiga, na wanyama wengine wadogo. Hifadhi ya Tarangire, ni maarufu kwa idadi kubwa ya tembo na miti ya baobab. Mto Tarangire unavuka hifadhi hii na kuwa chanzo cha maji kwa wanyama wengi wakati wa kiangazi, hivyo kuvutia wanyama wengi kwenye mto huo. OLDUVAI GORGE Olduvai Gorge ni bonde la kihistoria lililoko katika eneo la Ngorongoro. Eneo hili lina umuhimu mkubwa wa kiakiolojia kwani lilikuwa mojawapo ya maeneo ya kwanza duniani ambapo mabaki ya kale ya binadamu yaligunduliwa. Akiolojia ya Olduvai Gorge ilifanya eneo hili kuwa moja ya sehemu muhimu za kutembelea kwa watalii wanaopenda historia ya mwanzo wa binadamu. Watalii wanaweza kutembelea makumbusho ya eneo hilo na kujifunza zaidi kuhusu ugunduzi wa mabaki ya kale ya Homo Habilis. UTALII WA KITAMADUNI Arusha inajulikana pia kwa utajiri wa tamaduni za wenyeji, hasa Wamasai, Wachaga, na makabila mengine yanayoishi katika eneo hilo. Watalii hupata fursa ya kutembelea vijiji vya kienyeji na kujifunza kuhusu mila, desturi, na mitindo ya maisha ya jamii hizi. Mfano halisi ni kijiji cha Mto wa Mbu, ambacho kimejipatia umaarufu kama kituo cha utalii wa kitamaduni. Katika kijiji hiki, watalii wanapata nafasi ya kujionea, ngoma na muziki wa kitamaduni, vyakula vya kienyeji vinavyopikwa na wenyeji. Watalii pia hupata fursa ya kushiriki katika shughuli za kilimo cha kiasili na kuona jinsi jamii hizi zinavyohusiana na ardhi yao. Utalii wa Arusha unachangia kwa kiasi kikubwa kwenye ustawi wa jamii, uchumi wa mji, na maendeleo ya kijamii. Hapa chini kuna faida za utalii wa Arusha kwa jamii, na taifa kwa ujumla. AJIRA NA USTAWI WA KIUCHUMI Utalii ni moja ya vyanzo vikubwa vya ajira kwa wakazi wa Arusha. Sekta hii inatoa ajira nyingi moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja; ikiwemo, maafisa wa utalii, waongoza watalii, madereva, wapishi, na wahudumu katika hoteli mbalibali. Wafanyabiashara, kama vile wasanii wa kuchonga vinyago, wapishi wa vyakula vya kienyeji, na wauzaji wa bidhaa za kitamaduni pia almaarufu kama “cultures”, makampuni ya usafiri huajiri watu katika nyanja za usafirishaji na huduma za ziada kwa watalii. Kwa mfano, eneo la Mto wa Mbu limeweza kuendeleza sana biashara ya utalii wa kitamaduni, ambapo jamii hujishughulisha na biashara ya bidhaa za sanaa za mikono, na kilimo cha mazao yanayotumiwa kwenye migahawa inayohudumia watalii. Utalii pia, unaongeza mahitaji ya bidhaa na huduma mbalimbali kama vile vyakula, mavazi, na sanaa za mikono. Hii inatoa fursa kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati kuuza bidhaa zao kwa watalii. Maduka ya sanaa, migahawa ya kitamaduni, na biashara za usafiri zinakua kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaotembelea Arusha. MAENDELEO YA MIUNDOMBINU. Utalii umesababisha uboreshaji mkubwa wa miundombinu katika eneo la Arusha. Serikali na wawekezaji binafsi wamewekeza katika kuboresha barabara, huduma za afya, usafiri wa anga (uwanja wa ndege wa Arusha na wa kimataifa wa Kilimanjaro), na mawasiliano. Miundombinu hii haifaidishi watalii pekee, bali pia jamii inayozunguka, barabara bora zinaweza kutumiwa na wakazi kwa shughuli za kila siku, huduma za afya zinazoboreshwa kwa ajili ya watalii, kama hospitali na kliniki, pia hutumika na wakazi wa eneo hilo. Uwepo wa huduma za kisasa za mawasiliano kama vile mtandao wa kasi kama 5G na 4G kwenye mitandao mbalimbali ya simu, imerahisisha mawasiliano na hata kuchangia pia katika kutangaza utalii wetu. UHIFADHI WA MAZINGIRA Utalii unachangia kwenye uhifadhi wa mazingira kupitia hifadhi za taifa na maeneo ya asili. Watalii hulipa ada za kuingia katika hifadhi kama Ngorongoro, Serengeti, na Hifadhi ya Taifa ya Arusha, ambazo hutumika kwa ajili ya kuhifadhi wanyamapori, mimea, na mazingira. Pesa zinazokusanywa pia hutumiwa kwa miradi ya kijamii inayohusiana na mazingira, kama vile upandaji miti na elimu ya uhifadhi kwa wakazi wa maeneo jirani. Mfano halisi ni kupitia miradi kama ya Tanzania National Parks (TANAPA), ambapo jamii hunufaika kutokana na fedha zinazokusanywa kwa watalii. Hii inasaidia pia kudhibiti ujangili na uharibifu wa misitu.

KITOVU CHA UTALII TANZANIA Read Post »

FAHAMU MAANA, CHANZO, FAIDA NA HASARA ZA UTANDAWAZI KWA KIJANA KATIKA SHUGHULI ZAKE

By Debora K. Mwangosi Maana ya utandawazi. Utandawazi ni neno linalorejelea mchakato wa kuunganishwa kwa mataifa, tamaduni, na uchumi kupitia mtandao wa teknolojia, biashara, na mawasiliano. Ni hali ambapo mipaka ya kimataifa inakuwa dhaifu ambapo watu, bidhaa, na mawazo yanaweza kusafiri kwa urahisi zaidi kati ya nchi tofauti. Utandawazi unahusishwa na ongezeko la biashara ya kimataifa, mtandao wa dijitali, na ushawishi wa utamaduni wa kisasa. Chanzo cha utandawazi. Chanzo cha utandawazi kinaweza kufuatiliwa nyuma ya mabadiliko kadhaa makubwa katika historia. Kwanza, kuanzishwa kwa teknolojia ya mawasiliano kama vile simu, barua pepe, na mtandao wa intaneti kumefanya mawasiliano kuwa rahisi zaidi kati ya watu wa mataifa tofauti. Pili, mabadiliko katika sera za kiuchumi, kama vile uhuru wa kibiashara, yamewezesha nchi nyingi kufungua milango kwa biashara na uwekezaji wa kigeni. Aidha, utandawazi umechochewa na ukuaji wa usafiri wa kimataifa, kwa mfano usafiri wa anga ambao umepunguza matumizi ya muda mwingi kusafiri. Mifano ya utandawazi ni pamoja na kampuni kubwa za kimataifa, kama vile Google na McDonald’s, ambazo zina matawi katika nchi nyingi, na hivyo kuchangia katika kueneza utamaduni wa kisasa na bidhaa zao duniani kote. Kwa hivyo, utandawazi ni mchakato wa kihistoria unaoendelea, uliojaa fursa na changamoto ambazo kwa pamoja zinachangia katika kuunda ulimwengu wa kisasa wenye watu wanaoshirikiana zaidi kuliko wakati mwingine wowote katika historia. Sababu za Kutegemea Utandawazi kwa Vijana. Upatikanaji wa Habari na Mawasiliano: Utandawazi umepunguza vikwazo vya mawasiliano, na hivyo vijana wanaweza kupata habari na maarifa kwa urahisi kupitia mitandao ya kijamii. Hii inawasaidia kujifunza na kubadilishana mawazo kwa haraka. Fursa za Kazi na Ujasiriamali: Utandawazi umekuwa na mchango mkubwa katika kuunda fursa nyingi za kazi na biashara. Vijana wanaweza kutumia teknolojia na mitandao ya kijamii kujenga biashara zao, kufikia wateja wa kimataifa, na kujenga mtandao wa kitaaluma. Ushirikiano wa Kimataifa: Vijana wanapata fursa ya kushiriki katika miradi ya kimataifa, kubadilishana utamaduni, na kujifunza kutoka kwa watu wa tamaduni tofauti. Hii inawapanua wigo wa mawazo na mtazamo wa maisha. Mabadiliko ya Kijamii: Utandawazi unachochea mabadiliko ya kijamii na kisiasa, ambapo vijana wanakuwa na sauti katika masuala yanayowahusu. Kwa mfano, wanaweza kutumia mitandao ya kijamii kuhamasisha na kujadili masuala ya kijamii. Njia Ambazo Utandawazi Unamsaidia Kijana Katika Kuendesha Shughuli Zake Katika Jamii. Upatikanaji wa Maarifa na Ujuzi: Utandawazi unamwezesha kijana kupata mafunzo na taarifa kutoka vyanzo mbalimbali, kama vile mitandao ya kijamii, video za mafunzo, na makala mtandaoni. Hii inamsaidia kujifunza ujuzi mpya na kuwa na maarifa yanayohitajika katika shughuli zake. Kujenga Mtandao wa Kitaaluma: Kijana anaweza kuungana na watu wa fani mbalimbali duniani kote kupitia mitandao ya kijamii na majukwaa ya kitaaluma kama LinkedIn. Hii inamwezesha kuunda mahusiano ambayo yanaweza kumsaidia katika kupata nafasi za kazi au ushirikiano wa kibiashara. Fursa za Kazi na Ujasiriamali: Utandawazi unatoa fursa za kazi katika sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kazi za mbali (remote work). Vijana wanaweza pia kuanzisha biashara zao kwa kutumia majukwaa ya mtandaoni, kufikia wateja wa kimataifa. Mawasiliano na Ushirikiano: Utandawazi unarahisisha mawasiliano kati ya vijana na wadau mbalimbali katika jamii. Hii inawasaidia kushirikiana katika miradi ya kijamii, kujadili masuala muhimu, na kuhamasisha mabadiliko chanya. Baadhi Ya Madhara Ya Utandawazi Kwa Kijana. Mabadiliko ya Kitamaduni: Kijana anaweza kukumbana na mabadiliko ya haraka katika tamaduni, na hii inaweza kusababisha upotevu wa utamaduni wa nyumbani au kutokuelewana kati ya vizazi. Kwasababu utamaduni wao unakinzana na wa nyumbani. Matarajio ya Kazi: Utandawazi unaleta ushindani mkubwa katika soko la ajira, na kijana anaweza kujikuta katika mazingira magumu ya kupata kazi bora, hasa katika sekta zinazoendelea. Hii ni kwasababu utandawazi mara nyingi unakuwa unahitaji rasilimali watu kidogo. Athari za Kijamii: Kijana anaweza kuwa katika hatari ya kuathiriwa na mitindo hasi ya kijamii, kama vile matumizi mabaya ya dawa au tabia mbaya, kutokana na ushawishi wa mazingira ya mtandaoni. Wakati mwingine, kubadilisha mfumo wa maisha ya kuiga mwingine huchangia. Mabadiliko ya Maadili: Kutokana na ushawishi wa vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, kijana anaweza kukumbana na changamoto za maadili na maamuzi magumu kuhusu maisha yake. Ni muhimu kwa vijana kuwa na ufahamu wa changamoto hizi na na kukabiliana nazo ili waweze kufaidika na fursa za kiutandawazi. Matumizi Mabaya ya Teknolojia: Wakati vijana wanapokuwa na uwezo mkubwa kwa teknolojia, kuna hatari ya matumizi mabaya, kama vile uraibu wa michezo ya video au mitandao ya kijamii, ambayo inaweza kuathiri afya yao ya akili na mwili. Kukosekana kwa Ustadi wa Maisha: Vijana wanaweza kutegemea teknolojia kwa ajili ya kila kitu, na hivyo kukosa ustadi wa maisha kama vile mawasiliano ya ana kwa ana, ushirikiano, na uamuzi wa kibinafsi. Ewe kijana, ni muhimu kuwa na ufahamu wa athari hizi na kujenga ujuzi wa kukabiliana nazo. Kutafuta usaidizi, kujenga mitandao ya kijamii yenye afya, na kuzingatia maadili na tamaduni husika kunaweza kusaidia katika kuendesha maisha yenye maana na mafanikio katika ulimwengu wa utandawazi. Sambamba na hayo ujuzi wa nini cha kukiendea katika mitandao ni muhimu ili kuepuka changamoto zinazoweka kuepukika. Waswahili wanasema, heri nusu shari kuliko shari kamili.

FAHAMU MAANA, CHANZO, FAIDA NA HASARA ZA UTANDAWAZI KWA KIJANA KATIKA SHUGHULI ZAKE Read Post »

ZITAMBUE MBINU NA FAIDA ZA KUSOMA VITABU

By Jamal H. Maherea Kusoma vitabu kuna faida na manufaa mengi kwa mtu binafsi na jamii kwa ujumla.  Kujizoesha kusoma vitabu ni hatua muhimu ya kujenga tabia ya kujifunza na kuboresha ujuzi wa lugha, fikra, na maarifa.  Manufaa haya yanamfanya msomaji kuwa na mtazamo mpana, mwerevu zaidi, na mwenye uwezo bora wa kufikiri kwa makini na kuchanganua masuala. Hizi ni mbinu chache za kujizoesha kusoma vitabu kwa urahisi na ufanisi: 1. Weka malengo madogo ya kusoma. Anza kwa kuweka malengo yanayoweza kufikiwa, kama kusoma kurasa 10 au 20 kwa siku. Malengo haya madogo yatakusaidia kujenga tabia ya kusoma taratibu bila kusikia uzito. Ukiweka malengo makubwa yatakukatisha tama ukishindwa kuyafikia na kupelekea kutokuendelea na usomaji wa vitabu. 2. Chagua vitabu unavyovutiwa navyo   Soma vitabu vinavyokufurahisha au vinavyohusiana na maslahi yako binafsi. Unapoanza na vitabu unavyopenda, kusoma kunakuwa rahisi zaidi na unapata motisha ya kuendelea.  3. Panga muda maalum wa kusoma kila siku na unda mazingira mazuri ya kusoma Weka muda maalum kila siku kwa ajili ya kusoma. Inaweza kuwa asubuhi, mchana, au kabla ya kulala. Kufanya hivi kutakusaidia kujenga utaratibu wa kudumu. Tafuta sehemu tulivu na yenye mwanga mzuri ambapo unaweza kusoma . Ondoa vishawishi kama simu au TV ili uweze kujikita kikamilifu kwenye kitabu. 4. Fanya kusoma sehemu ya ratiba yako  Ongeza muda wa kusoma kwenye ratiba yako ya kila siku kama sehemu ya shughuli zako. Hata kama ni dakika 15 au 30, hiyo inatosha kukuza tabia ya kusoma.  5. Jitunze na thamini maendeleo yako Kila unapomaliza kitabu au kufikia lengo la kusoma, jitunze kwa kitu kidogo kama zawadi au pumziko la kujipongeza. Hii itakupa hamasa ya kuendelea na mpango wako wa kusoma. Kwa kutumia mbinu hizi, utaweza kuunda na kuimarisha tabia ya kusoma vitabu, na polepole utaanza kuona faida kubwa ya maarifa na ustadi unaopata kupitia kusoma. Tuzitambue faida za kusoma vitabu: Kuongeza maarifa:  Vitabu ni vyanzo vikubwa vya elimu. Kusoma vitabu kunakupa taarifa, maarifa, na uelewa wa masuala mbalimbali kama vile historia, sayansi, siasa, na utamaduni. Kuwa na utajiri wa maarifa ni nyenzo muhimu sana ya kukabiliana na changamoto pindi zinapojitokeza maishani mwako. Kufikirisha na kuchochea ubunifu:  Vitabu, hasa vya hadithi au falsafa, vinaweza kuchochea mawazo ya ubunifu na kukuza uwezo wa kufikiri kwa undani na kwa njia tofauti. Kuimarisha umakini na kumbukumbu:  Kusoma vitabu kunahitaji umakini, jambo ambalo linaimarisha uwezo wa kujilenga, kuzingatia, na kuboresha kumbukumbu. Kupunguza msongo wa mawazo:  Kusoma vitabu, hasa vya kuburudisha au vya kujenga fikra, husaidia kupumzisha akili na kupunguza mawazo ya msongo wa maisha ya kila siku. Kuboresha uwezo wa kutatua matatizo: Vitabu vingi vya kihistoria, kisaikolojia, au vya mbinu za maisha vinatoa maarifa kuhusu jinsi ya kutatua changamoto mbalimbali za maisha. Kuwa sehemu ya kikundi cha kusoma vitabu au forum za online: Hii itakupa motisha zaidi, kwani utakuwa na watu wa kubadilishana nao mawazo, na mara nyingi watakusaidia kushikilia utaratibu wa kusoma. Karibu katika website yetu kusoma makala tofauti tofauti zenye faida nyingi na kukujuza mambo mengi yatakayokujenga katika msingi mzuri zaidi na maadili mema.

ZITAMBUE MBINU NA FAIDA ZA KUSOMA VITABU Read Post »

Sifa 10 za mbuni zinazomtofautisha na ndege wengine

By Nasibu Mahinya Ukimshangaa mbuni asiyepaa utamstaajabu ngwini (pengwini); samaki asiyepaa mwenye uwezo wa kuogelea. Kawaida ukimkuta mbuni ndani ya hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro anavyovimba akiwa amejichanganya na pundamilia na nyumbu, wakitafuta malisho unaweza kusahau kuwa huyu ni ndege. Watu wengi wamekuwa wakimuona mbuni kama ndege wa kipekee na wa tofauti basi kama unaisoma hii makala utaweza kuujua utofauti kati ya mbuni na ndege wengine kupitia sifa zake 10. Twenzetu! 1. Muonekano Mbuni ndiyo ndege mrefu, mkubwa na mzito zaidi duniani. Ni mnyama mrefu kuliko wanyama wengine duniani. 2. Mfumo wa mmeng’enyo wa chakula Mbuni ana matumbo matatu na ni ndege pekee ambaye haja zake ndogo na kubwa hutoka tofauti, yani hazichangamani. 3. Mbio na kasi Mbuni anauwezo wa kukimbia kwa kasi ya kilomita 70 kwa saa, kasi kubwa kuliko ndege yoyote yule. Hivyo safari yake ya Dar kwenda Bagamoyo inaweza kumchukua saa moja tu. Hatua yake moja ni sawa na hatua tano za binadamu. Anaweza kuwa na wastani wa kilo 50 kama mbuzi vile lakini pia ana uzito sawa na jumla ya kuku 20. Hii ni ndiyo sababu kuu kwanini mbuni hana uwezo wa kupaa.  Sasa utajiuliza, kwanini kuku ni mwepesi lakini hapai juu angani kama kunguru? Naomba huo uwe mjadala wa siku nyingine. 4. Vidole Mbuni ana vidole viwili tu vya miguuni. Tofauti na ndege wengine wenye vidole vinne ambapo vitatu huangalia mbele na kimoja nyuma, mbuni ana vidole viwili kwenye mguu wake mmoja na vyote vinaangalia mbele. 5. Kujihami Kwenye hatari, silaha kubwa ya mbuni huwa ni mateke yake, hurusha mateke ya mbele yenye uwezo wa kuua wanyama wakali kama fisi, chui hadi simba. 6. Tabia za misimu Katika msimu wa masika mbuni hukaa peke yake ama akiwa na mpenzi wake. Katika msimu wa kiangazi, mbuni hukaa katika makundi ya mbuni wengi hadi 50. Wakati mwingine ndege hao hujichanganya na wanyama wengine kama pundamilia na swala. 7. Mapenzi yao ni ya kipekee Katika kitengo hiki, mbuni ana utaratibu wa kipekee sana. Kwanza jogoo la mbuni hupiga mabawa yake kama anataka kupaa ikiwa ni ishara kwamba anatafuta mwenza.  Akishapata mwenza, wanaanza kutafuta malisho na anahakikisha anampeleka sehemu ambapo hakuna wanyama wengine na wanaendelea kutafuta malisho hapo huku wakizoeana tabia.  Baadaye jogoo la mbuni huanza tena kupiga mabawa kwa nguvu zaidi na kuzunguka akiwa ameyashusha na akiwa anadonoa udongo, ambapo jike la mbuni likishaona hizo ishara basi huchuchumaa na kurusu kupandwa. 8. Yai la mbuni ni bonge la yai Mbuni zaidi ya mmoja huweza kutaga mayai yao kwenye tundu moja na kila mbuni ana uwezo wa kutofautisha mayai yake na ya mbuni wengine.  Yai la mbuni lina uzito wa zaidi ya kilo 1 na ukubwa sawa na nazi. Yai la mbuni bwana, unaweza kulikaangia viazi alimaarufu kwa chipsi mayai sahani kama tano hivi. 9. Jike na dume wote huatamia mayai Jike la mbuni ana rangi ya kijivu na huatamia mayai mchana kwa sababu rangi yake hufanana na mchanga hivyo ni ngumu kuonekana, huku jogoo la mbuni lenye rangi nyeusi hutamia mayai usiku kwa sababu ni ngumu kuonekana gizani. Mayai ya mbuni huchukua siku 35 mpaka 45 kutotolewa. 10. Jicho kubwa sana Jicho la mbuni linalingana na yai la kuku. Jicho la mbuni ni kubwa kuliko ubongo wake. Hivyo ana uwezo mkubwa sana wa kuona mbali na kwenye giza. Mbuni ni mnyama asiyeonekana kirahisi kwa sababu idadi yao imepungua sana hivyo kuwaona ni mpaka mbugani, kwenye hifadhi au kwenye mashamba ya watu binafsi wanapofugwa. Ukitaka kumuona mbuni basi tufunge safari moja kwa moja mpaka kwenye hifadhi za taifa za Serengeti, Mikumi, Ruaha au Katavi. Pia ukitembelea maeneo ya uhifadhi kama Selous na Ngorongoro utaweza pia kujionea mbuni.

Sifa 10 za mbuni zinazomtofautisha na ndege wengine Read Post »

Fisi: Mnyama wa ajabu kuliko tunavyodhani

By Nasibu Mahinya Inajulikana kwamba fisi akishika windo lake haachi kitu, anakula kuanzia kichwa hadi kwato. Dah! Hongera zake kwa kweli, maana mimi kila nikiwaza ng’ombe anapochinjwa kuna viungo vyake vingi huwa havifiki mezani. Fisi amethibiti upotevu usiyo na tija, wazungu wanaita ‘total diet.’ Hata asiyemjua fisi atakuambia jinsi mnyama huyo alivyopewa sifa ya kula kwenye hadithi na vitabu vingi lakini kama umekuja hapa kusoma hii makala, basi amini kwamba kuna mengi zaidi yatakayokuacha mdomo wazi. Binafsi kuandika tu hii makala, nikajikuta namshangaa fisi kama simjui vile wakati nishakutana naye mbugani mara nyingi tu; ni muoga tu hana lolote! Fisi ni mnyama jamii ya paka, ana ngozi ya njano ama kahawia mpauko yenye mabaka meusi. Hupenda kula wanyama wengine na huwinda kwa makundi. Fisi kala fisi! Jambo moja la kushangaza ni kwamba fisi anaweza kula fisi mwenzie. Kama vitoto vimezaliwa halafu ndiyo njaa imetawala basi hao ni chakula cha baba, kwani shida iko wapi? Si watazaa tu wengine!!! Na endapo akilipania windo hakubali kushindwa kirahisi, lazima atalipata. Ikiwa mnyama huyu amekula akashiba atalala lakini ikatokea ghafla wanakikundi wenzake wamemkamata nyumbu lazima ataamka na kujitapisha chakula alichokula ili tumbo lipate nafasi ya kumuweka nyumbu. Ndiyo maisha ya fisi hayo, mdomo ukiwa bize basi kwake yeye ndo ‘kasha-win’ maisha. Fisi jike ndiye masta, mbabe kuliko dume. Ana umbo kubwa na ni mkali zaidi kwenye suala la uwindaji. Fisi jike na fisi dume wote wawili wana uume. Uume wa dume hutumika katika kujamiiana ambapo huingia ndani ya uume wa jike. Kwa upande mwingine, uume wa jike hutumika kwenye uzazi na huishia kuchanika wakati anazaa. Katika uzazi, uume wa jike humpitisha mtoto na kwa kuwa ni mdogo basi mtoto wa fisi anaweza kupoteza maisha kwa kukosa hewa wakati anapitishwa kwenye uume huo. Fisi jike ana chuchu mbili tu ambazo watoto hugombania kunyonya hadi kuuana. Yaani mtoto wa fisi anapitia shuruba nyingi sana mpaka anakuja kuwa mkubwa na ndiyo maana hawezi kukubali kufa kizembe eti fisi afe kwa njaa, kweli!? Wako radhi hata wale viatu vya ngozi vilivyosahaulika na watalii kunusuru uhai, hivyo fisi hujitosa tu. Inasemekana kuwa fisi ana uwezo wa kufikiria kuliko sokwe. Hupenda kuiba mayai ya wanyama wengine kama mbuni. Yai la mbuni huwa ni ngumu kwa yeye kulipasua kwa meno yake hivyo basi hutafuta bonde lenye mawe au miamba, na yeye akiwa kwenye mwinuko, kisha huliachia yai hilo literemke na kupigiza kwenye mawe na miamba. Hufanya hivyo mara nyingi mpaka yai lipasuke ili aweze kula kilichomo ndani. Fisi hashindwi kwenye kula. Ni wanyama wa usiku, wanaishi kwenye nyasi, misitu, vichaka, jangwani na hata milimani. Wanyama hao ni waoga lakini umoja wao huwafanya kumshinda adui kwa urahisi na kula nyama yake bila kusalia kitu. Ukisikia kicheko porini amini kwamba hapo kuna hatari. Fisi hucheka kama mshangao akiona chakula. Fisi huwinda kwa makundi na fisi mwenye kicheko kikali zaidi ndiyo kiongozi wa kundi; na mara nyingi kundi huongozwa na fisi jike. Fisi dume hutimuliwa kwenye familia akishafikia balehe na hapo ndipo hujiunga na kundi la uwindaji na ni lazima apigane na fisi dume wa kundi hilo, na muda mwingine hupigana hadi kupoteza maisha. Fisi ni muoga sana akiwa peke yake, hana ujanja mwingi. Awapo mwenyewe hula watoto wa wanyama karibu wote uwajuao, kuanzia simba, chui, tembo hadi kifaru kwa sababu ana uwezo wa kuwamudu ila wakiwa kikundi wanakuwa na nguvu sana na kujiamini. Kundi la fisi linaweza kupigana na kundi la simba bila uwoga kabisa. Zamani fisi walikuwa wanahushishwa na ushirikina kwamba wachawi huwapanda kama farasi na kuwatumia kama usafiri wakienda kuiba watoto wa mifugo.  Fisi wanapatikana karibu kila mbuga hapa nchini na kama tulivyosema hapo awali, fisi huishi kwenye nyasi, misitu, vichaka, jangwani na hadi milimani. Tembelea Ngorongoro ujionee kwa macho yako mishemishe za fisi kutafuta mawindo mbugani. Tukutane tukiwa tumeenda mnara! Fisi hufanya mikutano ya kuwasiliana ambayo majike na madume wote huudhuria huku wakiwa wamesimamisha uume wao. Wanasayansi wanaamini kwamba uume wao huwasaidia kuwasiliana. Binafsi, naomba huu uwe mjadala mpana wa siku nyingine tafadhali. Hahahah! Ahsante.

Fisi: Mnyama wa ajabu kuliko tunavyodhani Read Post »

Pundamilia: Mnyama Mwenye Rangi Zenye Utata

By Nasibu Mahinya Siku ya kwanza namuona pundamilia ilikuwa mwaka 2002 kwenye banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika viwanja vya maonyesho ya biashara maarufu kama Sabasaba, jijini Dar es Salaam.  Nilikuwa nimeongozana na mama yangu mzazi ambaye alikuwa amenishika mkono kikakamavu huku nikitamani japo kuigusa ngozi ya mnyama huyo kwa sababu ilinivutia kuliko kawaida. Kwa bahati nzuri au mbaya, sikupata ruhusa ya kumshika na wala hata pundamilia mwenyewe asingekubali kushikwa na binadamu yeyote yule kwa sababu mnyama huyu anasifika kwa hulka ya woga. Ndugu msomaji, mimi nina swali kwako, pundamilia ni mnyama mweusi mwenye mistari myeupe au ni mnyama mweupe mwenye mistari myeusi?.  Tafakari kidogo.  Tayari?  Ok, vizuri!  Kama umewahi kusikia msemo usemao shukrani ya punda ni mateke, basi utafahamu dhahiri kuwa wanyama hawa wa jamii ya farasi na punda wana nguvu za ziada kwenye miguu yao. Sasa tuanze kwa kumuelewa vyema kabisa mnyama pundamilia kisha baadae nikupe majibu ya hilo swali. Pundamilia ni mnyamapori jamii ya farasi ambaye kitaalamu huangukia kwenye familia ya kinasaba kiitwacho ‘Ekwidae’ pamoja na farasi na punda.  Aina za pundamilia:  Kuna aina tatu za pundamilia zijulikanazo kitaalamu. Aina ya kwanza ni Pundamilia Grevi. Pundamilia hawa wana nguvu na ni wapole mithili ya punda na hapo zamani walitumika kubeba mizigo na kuvuta maguta. Wana umbo kubwa kuliko aina nyingine za pundamilia na huishi zaidi kwenye maeneo yenye ukame. Pundamilia wa milimani ni aina yao ya pili. Hawa ni pundamilia ambao huishi milimani kama jina lao lilivyo. Wana umbo dogo kuliko aina zote za pundamilia na hawana mistari tumboni. Pundamilia hawa huishi kwenye makundi madogo na mara nyingi dume humiliki majike kadhaa na kuishi nao huku madume wengine wakijitenga katika makundi yao. Aina nyingine ni pundamilia wa Savanna. Hawa ni pundamilia wanaoishi kwenye maeneo tambarare na ndiyo aina ya pundamilia wanaopatikana kwa wingi kuliko aina zote. Pundamilia hawa hupatikana kwa wingi kwenye mbuga na hifadhi zetu za Taifa. Wengi wao wana mistari hadi tumboni. Binadamu wameshajaribu sana lakini pundamilia hafugiki. Muonekano wake halisi: Ukweli ni kwamba pundamilia ni mnyama pori mweusi mwenye mistari myeupe kwa kuwa ngozi yake ni nyeusi iliyofunikwa na manyoya meusi na meupe. Pundamilia akinyolewa manyoya yake anabakia kuwa kiumbe mweusi.  Pundamilia anaweza kuwa na rangi nyeupe au kahawia iliyofifia pale mazingira yanapochangia kupauka huko au anapokuwa na ulemavu wa ngozi. Kama zilivyo alama za vidole vya binadamu, huwezi kukuta pundamilia wawili wanafanana, hata pundamilia pacha hawafanani.  Pundamilia huwa na uzito wa kuanzia kilo 200 mpaka kilo 400 na hii humfanya kuwa chakula pendwa cha wanyama wawindaji kama chui na simba kwa sababu ya kuwa steki ni ya kutosha.  Maisha yake: Kwa wastani mnyama huyu huishi miaka 20 mpaka 30 na ndama wa pundamilia huweza kutembea dakika takribani 20 baada ya kuzaliwa na hupata uwezo wa kukimbia baada ya saa kadhaa tu.  Pundamilia hukimbia kasi ya kilomita 60 kwa saa, hii inamaanisha kama akiamua kusafiri kutoka Dar es Salaam kuelekea Bagamoyo kwa kasi hiyo atatumia muda wa takribani saa moja. Pundamilia anapoona hatari, njia yake ya kwanza ya kujilinda ni kukimbia. Njia ambayo mara nyingi huwa haimsaidii kwa sababu wanyama wawindaji kama simba, chui, duma na mbwa mwitu wote wana kasi kuliko pundamilia.  Hapo unapata kuelewa kwa nini pundamilia ni kitoweo pendwa mbugani ukilinganisha na swala ambaye ni moja kati ya wanyama 10 wenye kasi zaidi ardhini au nyati ambaye simba wenyewe wakiwa wachache hawamuwezi kutokana na nguvu alizonazo ng’ombe pori huyo. Pundamilia hawa hupatikana kwa wingi kwenye mbuga na hifadhi zetu za Taifa. Wengi wao wana mistari hadi tumboni. Tabia na hulka yake: Kila mwaka zaidi ya pundamilia 200,000 huhama kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Maasai Mara iliyopo nchini Kenya na msafara huo huongozwa na pundamilia mkongwe zaidi.  Pundamilia huongozana pia na nyumbu na swala kwenye msafara huo ambao pia wanyama wawindaji huufuata nyuma nyuma kwa siri kwa sababu kama kitoweo kinahama sasa kwa nini na wao wasikifuate kilipo. Zaidi ya simba 3,000 hufuatilia msafara huo kwa umakini sana. Pundamilia hujikusanya kwa makundi kwa ajili ya kujilinda na wanyama wakali porini.  Kujikusanya kwao pamoja huwafanya wanyama kama simba kutoona vizuri viungo vya miili ya pundamilia, hivyo pale anapojichanganya katikati ya kundi la pundamilia hukutana na mateke ambayo yanaweza kumfanya apoteze maisha. Kama umewahi kusikia msemo usemao shukrani ya punda ni mateke, basi utafahamu dhahiri kuwa wanyama hawa wa jamii ya farasi na punda wana nguvu za ziada kwenye miguu yao. Kitu ambacho kiliwafanya watu wa zamani kuwaamini wanyama hawa kusafirisha abiria na mizigo kwa umbali mrefu. Binadamu wameshajaribu sana lakini pundamilia hafugiki. Kitu kimoja ambacho binafsi nilishuhudia na nikastaajabu kwenye hifadhi ya Taifa ya Mikumi ni kwamba pundamilia hulala wima. Mimi nilishajaribu kulala wima, je wewe umeshajaribu? Ukijaribu nijulishe.

Pundamilia: Mnyama Mwenye Rangi Zenye Utata Read Post »

Scroll to Top