
By Neema Minanago
Wazazi wanawajibu mkubwa katika kulinda haki za mtoto.Watoto wana haki mbalimbali za msingi katika makuzi na maendeleo yao kwa mujibu wa sheria za nchi na haki za kimataifa kama vile Mkataba wa Haki za Mtoto wa Umoja wa Mataifa (UNCRC). Haki hizo zimewekwa katika makundi makuu manne ambayo yamebeka haki nyingine zote. Haki hizo ni;
- Kumpatia mtoto haki ya kuishi
- Kumpatia mtoto haki ya kulindwa
- Kumpatia mtoto haki ya kuendelezwa
- Kumpatia mtoto haki ya kushiriki/kushirikishwa
Matunzo (Huduma). Matunzo yanahusisha kutoa mahitaji ya msingi ya kila siku kwa mtoto. Wajibu wa wazazi katika matunzo ni:
- Kumpatia mtoto chakula bora, malazi salama, na mavazi ya heshima.
- Kuhakikisha mtoto anapata huduma za afya.
- Kumlea katika mazingira salama na yenye upendo.
- Kuonyesha upendo, kuwahudumia, na kuwapa faraja watoto wanapohitaji msaada wa kihisia.
Ulinzi. Watoto wanahitaji ulinzi dhidi ya hatari zote zinazoweza kuathiri ustawi wao kimwili, kijamii, kisaikolojia, kiroho. Wajibu wa wazazi katika ulinzi ni pamoja na:
- Kuwalinda dhidi ya ukatili wa kingono, kimwili, kisaikolojia, kutelekezwa.
- Kufuatilia marafiki, maeneo wanayokwenda, na shughuli zao za kila siku.
- Kushirikiana na taasisi kama shule, vyombo vya sheria, na ustawi wa jamii iwapo kuna hatari yoyote.
Wazazi wana nafasi ya kipekee katika maisha ya mtoto. Kwa kutimiza wajibu wao katika malezi, kulinda haki, kutoa matunzo na ulinzi, wanachangia si tu katika maendeleo ya mtoto binafsi, bali pia katika kujenga jamii yenye maadili, amani na maendeleo. Familia imara huzaa taifa imara.
FAMILIA NA MASWALA YA MALEZI KISHERIA
Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019 inaekeza bayana wajibu wa Mzazi/Mlezi katika kutoa Malezi, Matunzo na Haki kwa mtoto.
Kifungu Namba 8.-
(1) Itakuwa ni wajibu wa mzazi, mlezi au mtu mwingine yeyote anayemlea mtoto kumtunza mtoto huyo na jukumu hilo linampa mtoto haki ya-
(a) chakula
(b) malazi
(c) mavazi
(d) huduma ya afya pamoja na kinga
(e) elimu na muongozo
(f) uhuru, na
(g) haki ya kucheza na kupumzika.
(2) Mtu hatamnyang’anya mtoto haki ya kupata elimu, kinga, chakula, mavazi, malazi, huduma za afya au kitu chochote kinachohitajika kwa ajili ya maendeleo yake.
(3) Mtu hatamnyima mtoto haki ya huduma ya afya kwa sababu ya kidini au imani nyingine.
(4) Mtu hatamnyima mtoto haki ya kushiriki katika ichezo, au katika shughuli chanya za kiutamaduni na kisanii au katika shughuli nyingine za starehe isipokuwa kama kwa maoni ya mzazi, mlezi au ushiriki wa mtoto katika shughuli hizo si kwa maslahi yake.
(5) Mtu hatamtendea mtoto mwenye lemavu kwa namna ambayo si ya kiutu.
(6) Mtoto mwenye ulemavu atastahili uangalizi maalum, matibabu na huduma nafuu kwa ajili ya kumrekebisha na kupata fursa sawa katika elimu na mafunzo kwa kadri itakavyowezekana ili kuendeleza kipaji chake, uwezo wake na kuweza kujitegemea.
Kifungu Namba 9.-
(1) Mtoto atakuwa na haki ya kuishi, utu, heshima, mapumziko, uhuru, huduma za afya, elimu na malazi toka kwa wazazi wake.
(2) Haki ya mtoto kupumzika na kuwa huru itazingatia mwongozo na uwezo wa mzazi, mlezi au ndugu.
(3) Kila mzazi atakuwa na wajibu na majukumu yaliyowekwa ama na sheria au vinginevyo kwa mtoto wake ambayo yatajumuisha wajibu wa-
(a) kumlinda mtoto dhidi ya utelekezwaji, ubaguzi, urugu, unyanyasaji, madhara ya kimwili na kiakili na ukandamizaji
(b) kutoa mwongozo malezi, msaada na matunzo kwa mtoto na kuhakikisha uhakika wa mtoto kuishi na maendeleo “kuendelezwa”; na
(c) kuhakikisha kuwa kwa muda ambao mzazi hatakuwepo, mtoto atapata malezi toka kwa mtu anayefaa, isipokuwa tu pale ambapo mzazi amekabidhi haki na wajibu huo kwa mtu mwingine kulingana na sheria au kwa taratibu za kimila.
(4) Endapo wazazi wa mtoto wamefariki, jukumu la kumlea linaweza kuhamishiwa kwa ndugu au mlezi aliyeteuliwa kwa amri ya mahakama au kwa taratibu za kimila.
Kifungu Namba 10.
Mtu hatamnyang’anya mtoto haki ya kufaidia ipasavyo mali za wazazi. 11. Mtoto atakuwa na haki ya kutoa maoni na mtu yeyote hatamnyima mtoto mwenye uwezo wa kutoa maoni haki ya maoni, ya kusikilizwa na kushiriki katika maamuzi yatakayohusu maisha yake.
Kifungu Namba 12.
Mtu hatamuajiri au kumfanyisha mtoto kazi ambazo zinaweza kuwa na madhara kwa afya, elimu, akili, mwili au kwa maendeleo ya kimaadili ya mtoto.
Kifungu Namba 13.-
(1) Mtu hatamsababishia mtoto mateso, au aina nyingine ya ukatili, kumpa adhabu zisizo za kibinadamu au kumdhalilisha mtoto ikijumuisha mila na desturi zozote zenye madhara kwa mtoto kimwili au kiakili.
(2) Adhabu haitakuwa stahili kwa mtoto iwapo ni mbaya kwa aina yake au ni kubwa kwa kiwango chake kulingana na umri wa mtoto, hali ya mtoto kimwili na kiakili; na adhabu haitakuwa stahili kwa mtoto iwapo kutokana na umri mdogo wa mtoto au kwa sababu nyingine hawezi kuelewa lengo la adhabu hiyo.
(3) Istilahi “udhalilishaji” kama ilivyotumika katika kifungu hiki maana yake kitendo kinachofanywa kwa mtoto kwa nia au dhamira ya kumdhalilisha au kushusha hadhi yake. Adhabu 14. Mtu atakayekiuka kifungu chochote katika Sehemu hii atakuwa ametenda kosa na atakapotiwa hatiani atalipa faini isiyozidi shilingi milioni tano au kifungo cha miezi isiyozidi sita au vyote kwa pamoja.
Ulinzi wa mtoto: Kifungu Namba 17.-
(1) Mtu ambaye ni mmiliki au anaendesha au ni msimamizi wa ukumbi wa muziki, baa au klabu ya usiku, hatamruhusu mtoto kuingia katika maeneo hayo.
(2) Mtu hatamuuzia mtoto sigara, pombe, pombe kali, madawa ya kulevya au kitu chochote kinacholewesha.
(3) Mtu atakayekiuka masharti ya kifungu hiki, atakuwa ametenda kosa na atakapotiwa hatiani atalipa faini ya kiasi kisichopungua shilingi milioni moja na kisichozidi shilingi milioni tano au kifungo kwa kipindi kisichozidi miezi kumi na miwili au vyote kwa pamoja.
Kifungu Namba 158
- kimetoa katazo la jumla katika kuendelea kulinda haiba ya mtoto:
Mtu hata…
(a) tenda au kuagizwa kutendwa ukeketaji kwa mtoto
(b) chapisha, kutengeneza, kuonyesha au kuagiza kuchapishwa, kuendeshwa au kuonyeshwa picha au taswira ya mtoto au mtoto aliyefariki iliyoonyesha ukatili au katika pozi za ngono
(c) mtumia mtoto katika maonyesho ya harusi, maonyesho ya mitindo ya nguo au maonyesho mengine yoyote yanayofanana na hayo wakati wa usiku
(d) chapisha au agiza kuchapishwa taarifa yoyote ambayo inaathiri maslahi ya mtoto
(e) lazimisha mtoto aliyeasiliwa au mtoto aliye chini ya malezi ya kambo kubadili dini yake ya kuzaliwa; au
(f) tumia au agiza kutumika au kumhusisha mtoto aliye katika makao yaliyothibitishwa au taasisi kwa ajili ya kuomba omba au kwa ajili ya faida binafsi; na
(g) tumia vibaya msaada au aina nyingine ya msaada uliyolengwa katika kusaidia au kutunza watoto katika taasisi.
(2) Mtu yeyote atakayekiuka masharti yoyote ya kifungu kidogo cha (1), anatenda kosa na atakapotiwa hatiani atalipa faini isiyopungua shilingi laki tano au kifungo cha miezi sita au vyote kwa pamoja.
Majukumu ya msingi ya baba kama msimamizi mkuu wa familia yanaweza kutofautiana kulingana na mila, tamaduni, dini, na mazingira ya kijamii. Hata hivyo, kwa ujumla, baba katika familia anatarajiwa kutekeleza majukumu yafuatayo:
1. Kiongozi wa Familia: Bama ndani ya familiamara nyingi hupewa nafasi ya kuwa kichwa cha familia, akiongoza kwa busara, hekima na maadili. Ana jukumu la kuhakikisha familia inafuata mwelekeo mzuri wa maisha na kufanya maamuzi yanayolinda maslahi ya familia.
2. Mlezi na Mfano wa Kuigwa: Anapaswa kuwa mfano wa tabia njema kwa watoto na familia kwa ujumla. Tabia yake, maamuzi na namna anavyojieleza vinapaswa kuwa msingi wa malezi bora ya watoto.
3. Mtoaji wa Mahitaji ya Msingi: Babaanatakiwa kuhakikisha familia yake inapata mahitaji ya msingi kama vile chakula, mavazi, malazi, elimu, na huduma za afya. Ingawa nyakati za sasa wanawake pia wanachangia, mwanaume bado anabeba jukumu kubwa la kifamilia.
4. Mlinzi na Msimamizi wa Usalama wa Familia: Anapaswa kuhakikisha familia yake ipo salama kimwili, kihisia, na kiakili. Hili linahusisha kujiepusha na vitendo vya ukatili na kulinda familia dhidi ya madhara ya nje.
5. Mshauri na Mlezi wa Kiroho na Maadili: Katika jamii nyingi, baba ana wajibu wa kuhakikisha familia inafuata maadili mema, dini au imani, na mshikamano wa kijamii. Anaongoza familia katika kusali, kuheshimu watu na kufuata mila nzuri.
6. Mshiriki wa maswala ya Kifamilia: Anapaswa kushirikiana na mkewe katika malezi ya watoto na kushughulikia changamoto mbalimbali za kifamilia. Ushirikiano huu hujenga familia yenye mshikamano, upendo na amani.
7. Kusimamia Maendeleo ya Familia: Baba anatakiwa kuongoza familia kuelekea maendeleo – kielimu, kiuchumi na kijamii. Hii ni pamoja na kupanga mipango ya baadaye kama uwekezaji, elimu ya watoto, na ustawi wa familia kwa ujumla.
8. Kudumisha Mshikamano na Upatanisho Ndani ya Familia: Baba ana wajibu mzito wa kuwa mpatanishi na mleta mshikamano wakati wa migogoro ya kifamilia. Anatakiwa kutumia hekima kutatua tofauti baina ya yake na mkewe, kati ya watoto, au baina ya familia wana familia wengine ndugu jamaa na jamii. Kiongozi huyu wa familia ni kama nguzo ya amani, akihakikisha familia haivunjiki kwa sababu ya migogoro isiyotatuliwa.
9. Kujitolea kwa Ustawi wa Kizazi Kinachofuata (Intergenerational Responsibility): Baba kama mkuu wa familia ni mwenye maono hufanya maamuzi yanayolinda siyo tu familia ya sasa, bali pia kizazi kijacho. Anawekeza kwenye elimu, tabia, urithi wa mila njema, na ustawi wa kiuchumi wa watoto wake, kuhakikisha kwamba wana msingi imara wa maisha hata baada ya yeye kutokuwepo.
10. Kuwa Nguzo ya Maadili Katika Jamii: Zaidi ya familia yake, baba anabeba dhamana ya kuwa kielelezo cha maadili mema katika jamii. Kwa kufanya hivyo, anajenga heshima ya familia yake na kuchangia kwenye ustawi wa kijamii. Hili linahusisha kujiheshimu, kuwa mkweli, kuepuka rushwa, na kuwa tayari kusaidia wengine. Majukumu haya matatu yanamtaka baba awe na dhamira, busara, na moyo wa kujitolea si tu kwa familia yake bali pia kwa vizazi vya baadae na jamii kwa ujumla.
Majukumu ya msingi ya mama katika familia yanaweza kutofautiana kulingana na mila, tamaduni, dini, na mazingira ya kijamii. Hata hivyo, kwa ujumla, mama kama mlezi wa familia anatarajiwa kutekeleza majukumu yafuatayo:
1. Mlezi Mkuu wa Watoto Mama ndiye mwalimu wa kwanza. Analea watoto kwa maadili, kuwaelekeza katika njia ya heshima, utii, na bidii. Ana nafasi ya pekee katika kuunda tabia na mwelekeo wa maisha ya watoto.
2. Nguzo ya Upendo na Faraja Nyumbani Anatoa upendo, huruma, na uelewa unaojenga amani na mshikamano wa familia. Mwanamke anayejielewa hutuliza migogoro na kujenga mazingira salama ya kihisia kwa watoto na mume wake.
3. Mshirika wa Maendeleo ya Familia Anashirikiana na mume katika mipango ya kifamilia kama vile bajeti, elimu ya watoto, na maendeleo ya kijamii. Hachukui familia kama kazi ya mtu mmoja bali anakuwa mshirika kamili.
4. Msimamizi wa Maadili Nyumbani Anahakikisha nyumba inakuwa mahali pa maadili, ibada, nidhamu, na heshima. Anaelekeza watoto kutambua mema na mabaya, akishirikiana na baba katika kuwalea kiutu na kiroho.
5. Mlinzi wa Afya na Ustawi wa Familia Anachangia katika kuhakikisha chakula bora, usafi, na matibabu ya familia. Anafanya kazi kuhakikisha familia inaishi kwa afya bora.
6. Mhamasishaji wa Amani na Ushirikiano Mamahupatanisha migogoro midogo midogo, hutunza siri za familia, na kuhakikisha kila mmoja anasikia sauti yake ndani ya nyumba.
7. Mfano wa Kuigwa na Watoto wa Kike na Kiume Watoto humuangalia mama kama mwalimu wa maisha. Kwa hiyo, tabia, lugha, mavazi, na maamuzi ya mama yanakuwa somo kwa watoto wake siku zote.
8. Msimamizi wa Rasilimali Ndani ya Nyumba Anahakikisha matumizi ya rasilimali kama chakula, pesa, na muda yanakwenda vizuri. Hupanga, hupangilia, na hutunza vitu vya familia kwa uangalifu.
Hitimisho: Wazazi na walezi wana wajibu mkubwa wa kuongoza familia zao kwa maadili, upendo na mshikamano. Baba na Mama wanapaswa kushirikiana, si kushindana. Familia yenye usawa na uwajibikaji kutoka kwa wazazi huzaa watoto bora na jamii yenye amani.