By Jamal H. Maherea
Arusha ni mojawapo ya maeneo ya kipekee barani Afrika ambayo yamebarikiwa kuwa na vivutio vya kipekee vya utalii, ikiwemo hifadhi za wanyamapori, milima yenye mandhari nzuri, na tamaduni tajiri za wenyeji. Arusha ni mji unaounganisha urithi wa asili na utajiri wa utamaduni, na hivyo kuifanya kuwa kivutio muhimu kwa wale wanaotafuta uzuri wa asili wa Afrika Mashariki. Twende kutazamia baadhi ya vivutio vinavyoupamba mji wa Arusha na kuufanya kuwa kitovu cha utalii.
HIFADHI ZA TAIFA
Arusha ni kitovu cha safari za kitalii kutokana na ukaribu wake na hifadhi nyingi maarufu za taifa. Moja ya hifadhi maarufu duniani, Serengeti inayojulikana kwa tukio la uhamaji mkubwa wa nyumbu, ambapo nyumbu huenda kutafuta malisho mapya. Ngorongoro Crater ni kivutio cha kipekee ambacho ni volkano kubwa iliyozama na sasa ni makazi ya aina mbalimbali za wanyama, ikiwa ni pamoja na simba, faru weusi, tembo, na pundamilia. Watalii katika hifadhi ya Taifa ya Arusha, wanaweza kufanya safari za miguu (walking safaris), ambayo ni nadra kulinganishwa na hifadhi nyingine. Pia, hifadhi hii ni maarufu kwa nyani, twiga, na wanyama wengine wadogo.

Hifadhi ya Tarangire, ni maarufu kwa idadi kubwa ya tembo na miti ya baobab. Mto Tarangire unavuka hifadhi hii na kuwa chanzo cha maji kwa wanyama wengi wakati wa kiangazi, hivyo kuvutia wanyama wengi kwenye mto huo.
OLDUVAI GORGE
Olduvai Gorge ni bonde la kihistoria lililoko katika eneo la Ngorongoro. Eneo hili lina umuhimu mkubwa wa kiakiolojia kwani lilikuwa mojawapo ya maeneo ya kwanza duniani ambapo mabaki ya kale ya binadamu yaligunduliwa. Akiolojia ya Olduvai Gorge ilifanya eneo hili kuwa moja ya sehemu muhimu za kutembelea kwa watalii wanaopenda historia ya mwanzo wa binadamu. Watalii wanaweza kutembelea makumbusho ya eneo hilo na kujifunza zaidi kuhusu ugunduzi wa mabaki ya kale ya Homo Habilis.
UTALII WA KITAMADUNI

Arusha inajulikana pia kwa utajiri wa tamaduni za wenyeji, hasa Wamasai, Wachaga, na makabila mengine yanayoishi katika eneo hilo. Watalii hupata fursa ya kutembelea vijiji vya kienyeji na kujifunza kuhusu mila, desturi, na mitindo ya maisha ya jamii hizi. Mfano halisi ni kijiji cha Mto wa Mbu, ambacho kimejipatia umaarufu kama kituo cha utalii wa kitamaduni. Katika kijiji hiki, watalii wanapata nafasi ya kujionea, ngoma na muziki wa kitamaduni, vyakula vya kienyeji vinavyopikwa na wenyeji. Watalii pia hupata fursa ya kushiriki katika shughuli za kilimo cha kiasili na kuona jinsi jamii hizi zinavyohusiana na ardhi yao.
Utalii wa Arusha unachangia kwa kiasi kikubwa kwenye ustawi wa jamii, uchumi wa mji, na maendeleo ya kijamii. Hapa chini kuna faida za utalii wa Arusha kwa jamii, na taifa kwa ujumla.
AJIRA NA USTAWI WA KIUCHUMI
Utalii ni moja ya vyanzo vikubwa vya ajira kwa wakazi wa Arusha. Sekta hii inatoa ajira nyingi moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja; ikiwemo, maafisa wa utalii, waongoza watalii, madereva, wapishi, na wahudumu katika hoteli mbalibali. Wafanyabiashara, kama vile wasanii wa kuchonga vinyago, wapishi wa vyakula vya kienyeji, na wauzaji wa bidhaa za kitamaduni pia almaarufu kama “cultures”, makampuni ya usafiri huajiri watu katika nyanja za usafirishaji na huduma za ziada kwa watalii. Kwa mfano, eneo la Mto wa Mbu limeweza kuendeleza sana biashara ya utalii wa kitamaduni, ambapo jamii hujishughulisha na biashara ya bidhaa za sanaa za mikono, na kilimo cha mazao yanayotumiwa kwenye migahawa inayohudumia watalii.
Utalii pia, unaongeza mahitaji ya bidhaa na huduma mbalimbali kama vile vyakula, mavazi, na sanaa za mikono. Hii inatoa fursa kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati kuuza bidhaa zao kwa watalii. Maduka ya sanaa, migahawa ya kitamaduni, na biashara za usafiri zinakua kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaotembelea Arusha.
MAENDELEO YA MIUNDOMBINU.

Utalii umesababisha uboreshaji mkubwa wa miundombinu katika eneo la Arusha. Serikali na wawekezaji binafsi wamewekeza katika kuboresha barabara, huduma za afya, usafiri wa anga (uwanja wa ndege wa Arusha na wa kimataifa wa Kilimanjaro), na mawasiliano. Miundombinu hii haifaidishi watalii pekee, bali pia jamii inayozunguka, barabara bora zinaweza kutumiwa na wakazi kwa shughuli za kila siku, huduma za afya zinazoboreshwa kwa ajili ya watalii, kama hospitali na kliniki, pia hutumika na wakazi wa eneo hilo. Uwepo wa huduma za kisasa za mawasiliano kama vile mtandao wa kasi kama 5G na 4G kwenye mitandao mbalimbali ya simu, imerahisisha mawasiliano na hata kuchangia pia katika kutangaza utalii wetu.
UHIFADHI WA MAZINGIRA
Utalii unachangia kwenye uhifadhi wa mazingira kupitia hifadhi za taifa na maeneo ya asili. Watalii hulipa ada za kuingia katika hifadhi kama Ngorongoro, Serengeti, na Hifadhi ya Taifa ya Arusha, ambazo hutumika kwa ajili ya kuhifadhi wanyamapori, mimea, na mazingira. Pesa zinazokusanywa pia hutumiwa kwa miradi ya kijamii inayohusiana na mazingira, kama vile upandaji miti na elimu ya uhifadhi kwa wakazi wa maeneo jirani. Mfano halisi ni kupitia miradi kama ya Tanzania National Parks (TANAPA), ambapo jamii hunufaika kutokana na fedha zinazokusanywa kwa watalii. Hii inasaidia pia kudhibiti ujangili na uharibifu wa misitu.