Papa: Samaki Bubu Asiyelala

By Nasibu Mahinya

Hakuna kiumbe anaogopeka majini kama Papa!

Anapotajwa papa, vitu viwili huja akilini mwa wengi; maji na damu. Binafsi nilikuwa mmoja kati ya watu wanaoamini kwamba binadamu akikutana na papa basi amekwisha! 

Cha kushangaza zaidi ni kwamba hakuna uthibitisho kuwa papa huwinda binadamu lakini humshambulia pale anapoingilia himaya yake; papa hudata na kuchanganyikiwa.

Papa tunayemuogopa huchukua maisha ya binadamu mmoja tu kila mwaka, lakini ng’ombe tusiyemuogopa huchukua maisha ya binadamu 22 kila mwaka.

Mwanabaiolojia wa papa kutoka Marekani, marehemu Samuel Gruber aliweka wazi kwamba papa humuogopa binadamu kuliko viumbe wengine wote kwa sababu zaidi ya papa million 73 kila mwaka huuawa kutokana na migogoro baina ya binadamu na Wanyama, na wengine huvuliwa na binadamu na kutumika kama kitoweo.

Chakula kikuu cha papa ni samaki wadogo kama ngisi na viumbe vingine vya majini ingawa mara nyingi hachagui sana. Papa wakubwa hula viumbe wakubwa kama sili, pweza na taa.

Meno yao ni makali kama msumeno ambao humsaidia kuwinda. Hunyata kisha hung’ata na kunyofoa kabisa sehemu ya mwili ya windo lake na kukiacha kiumbe kikivuja damu na baadaye kukirudia kipande kilichobaki akijua dhahiri kwamba, windo lake haliwezi kujiokoa tena.

Kuna papa wa ajabu kweli duniani. Kuna zaidi ya aina mia tano za papa na ukiingia chini ya bahari utajionea baadhi. Hutoamini kuna papa wanaofanana na farasi, paka, mamba hadi pundamilia lakini pia kuna hadi papa mwenye kichwa kimekaa kama nyundo.

Papa jike anaweza kubeba ujauzito uliochangiwa mbegu na papa dume zaidi ya wawili.

Papa anaweza kuwa mjamzito kwa miaka miwili na kati ya aina mia tano za papa, asilimia 40 hutaga mayai, asilimia 60 huzaa. Huzaa eneo ambalo amezaliwa yeye, na watoto wake huwa na meno yao yote mdomoni. Papa mkubwa huota hadi meno 50,000.

Pamoja na sifa hizo nyingine kwa majike ni kwamba, wanauwezo wa kutunza mbegu za papa dume ambazo hazikutumika mara ya mwisho wanajaamiana na hivyo kuzitumia kipindi ambacho papa dume hayupo.

Mnyama huyo wa majini ana uwezo mkubwa wa kunusa lakini pia ana uwezo kusikia mapigo ya moyo ya viumbe wengine. Siyo papa wote huishi baharini, wengine huishi kwenye maziwa na mito mikubwa.

Papa ana uti wa mgongo ambao hauna mifupa, na uti wake hutengenezwa kwa misuli na gegedu. Gegedu ni mfumo wa mifupa ambayo haijakomaa, ni kama mifupa ya mtoto mchanga. Gegedu humsaidia papa kuogelea kwa spidi na kukunja kona za ghafla pale anapofukuzia windo lake.

Papa halali. Hutomkuta papa amelala usingizi hata siku moja, yeye hutulia tu na kupumzika kwenye mapango bila kuingia kwenye hali ya usingizi. Kutolala humfanya awe makini sana na mazingira yanayomzunguka ili aone hatari inapokaribia; na pia kuona fursa za mawindo zinapojitokeza.

Papa ni wanyama wakongwe, wamekuwepo duniani kwa miaka milioni 850 iliyopita na hapo zamani walikuwa wakubwa sana, kiasi cha kuwa na urefu wa futi 50 na uzito wa tani 25. Hili ni kama lori lenye ‘semi trella’.

Wapo pia papa wadogo wanaoweza kutosha kwenye kibakuli cha supu. Epuka kufuga papa kwenye tenki au bwawa moja na samaki wengine, atawafanya kitoweo bila kujali kwamba yeye na wenzake ni samaki wa mmiliki mmoja.

Moja kati ya viumbe ambao wamenyimwa uwezo wa kutoa sauti ni papa. Ni wakimya, hawatoi sauti hata kidogo. Ububu wa papa unawafanya wasiwasiliane sana, kitu ambacho kinawafanya kuwa samaki wa kujitenga ingawaje hujumuika pamoja wakati wa kuwinda. 

Tofauti na ilivyo kwa samaki wengi, papa hana magamba bali ana ngozi ila ngozi yake siyo laini, ina manundu madogo madogo kama msasa.

Jinsi ya kuwaona papa:

Ili kwenda kujionea maajabu ya dunia iliyopo chini ya bahari unaweza kufanya utalii wa kuzama baharini ukiwa na mitungi maalumu wa gesi yenye oksijeni. Utalii huu uwaweza kukutanisha na mnyama huyo kinara wa maji.

Siku ukipata fursa ya kwenda Zanzibar au Mafia na ukafanikiwa kufanya utalii huu unaofahamika kama ‘scuba diving’; na ukafanikiwa kukutakutana na papa huko chini baharini, basi zingatia sana lugha yao ya mwili.

Ukiona umeingia kwenye himaya ya papa na ukawaona wametulia na muda mwingine wakawa wanaendelea na shughuli, basi tambua kwamba hawawezi kukudhuru. Wakati mwingine wanaweza kukufuata na kucheza karibu nawe. Samaki hawa huwasiliana zaidi kwa kutumia lugha ya mwili.

Tahadhari! Ukiona papa amebinjua na kutunisha mgongo wake huku akiwa ametanua gego zake basi tambua kwamba hapo unapewa onyo, ondoka mapema la sivyo utakiona cha mtema kuni!!! 

Scroll to Top