
KAULI MBIU “MTOTO NI MALEZI: MSINGI WA FAMILIA BORA KWA TAIFA IMARA”
Tujifunze na Kufurahia Maarifa Mapya kwa Makala hii fupi ya Familia na Malezi
By Neema Minanago
Maana ya Familia:
Familia ni kikundi cha watu wanaohusiana kwa damu, ndoa, au kuasili, wanaoishi pamoja na kushirikiana majukumu ya kila siku kama vile malezi ya watoto, upendo, usaidizi wa kifamilia, maadili, imani, tamaduni na kushirikiana rasilimali. Familia ndiyo msingi wa jamii, kwani ndani yake ndipo mtoto hupata malezi ya awali, maadili, lugha, na utambulisho wa kijamii. Kwa lugha rahisi, familia ni sehemu ya kwanza kabisa ambayo mtu huzaliwa au kukua, na ambayo hutoa ulinzi, msaada wa kihisia na kimwili, na mwongozo wa maisha. Kwa mfano: Wazazi na watoto wao wanaoishi pamoja ni familia. Bibi, babu, na wajukuu wanaoishi pamoja pia ni familia. Mtu anayeasili mtoto na kumlea kama wake pia anaunda familia. Familia hubadilika kulingana na utamaduni, mazingira, na hali ya maisha, na hivyo kuna aina nyingi tofauti za familia leo hii.
Katika familia yenye afya na mshikamano, kila mzazi, mwanaume na mwanamke, ana nafasi ya kipekee. Mwanaume anayo nafasi ya kuwa kiongozi na mlinzi, huku mwanamke akiwa mhimili wa malezi, upendo, na maendeleo ya ndani ya familia. Familia zenye uwiano mzuri wa majukumu huzaa jamii zenye nidhamu, heshima, na maendeleo.
Aina za Familia
Familia ya Mzazi Mmoja (One Parent Family):
Hii ni familia inayojumuisha mzazi mmoja tu (mama au baba) pamoja na watoto wake. Hali hii huweza kusababishwa na talaka, kifo cha mzazi mwingine, au uamuzi wa mzazi mmoja kulea peke yake.
Familia ya Talaka (Divorced Family):
Hii ni familia ambayo wazazi wake wameachana rasmi kwa njia ya kisheria. Watoto wa familia hii huishi na mzazi mmoja au kugawanywa kati ya wazazi wawili kwa makubaliano maalum.
Familia Pana (Extended Family):
Familia hii inahusisha siyo tu wazazi na watoto, bali pia jamaa wengine kama babu, bibi, shangazi, mjomba, na binamu wanaoishi au kushirikiana maisha ya kifamilia.
Familia ya Watu wa Jinsia Moja (Homosexual Family):
Hii ni familia inayoundwa na watu wawili wa jinsia moja walioko kwenye uhusiano wa ndoa au mahusiano ya kudumu, na mara nyingi huwa na watoto kwa njia ya kuasili au teknolojia ya uzazi.
Familia ya Ndoa (Marital Family):
Hii ni familia inayoundwa na mume na mke walioko kwenye ndoa rasmi pamoja na watoto wao. Hii ndiyo aina ya familia iliyokuwa ya kawaida katika jamii nyingi.
Maana ya Malezi:
Malezi (Parenting): ni mchakato wa kulea, kuendeleza, kulinda, kuongoza, na kufundisha mtoto kwa upendo usio na masharti, maadili na nidhamu.kijamii, kiakili, kimwili, kiroho na kihisia tangu akiwa tumboni hadi kufikia utu uzima. Ni juhudi zinazofanywa na wazazi, walezi, jamii, au taasisi ili kumjenga mtoto awe mtu mwadilifu, mwenye maadili, anayejitambua, na mwenye mchango chanya katika jamii. Mzazi anapaswa kutumia nidhamu chanya (Positive Discipline) badala ya adhabu kali na kuzungumza na watoto badala ya kuwafokea pekee, kuwatukana na kuwaita majina yasiyofaa.

Vipengele Muhimu vya Malezi
- Kielimu – Kumpa mtoto maarifa na stadi muhimu kwa maisha.
- Kimaadili – Kumfundisha mema na mabaya, heshima, uaminifu, na uwajibikaji.
- Kihisia – Kumpa upendo, ulinzi, na msaada wa kihisia ili ajenge hali ya kujiamini.
- Kimwili – Kuhakikisha mtoto anapata chakula bora, afya njema, na mazingira salama.
- Kijamii – Kumwelekeza jinsi ya kuishi vizuri na watu, kuheshimu sheria na mila.
Aina za Malezi
- Malezi ya Kidemokrasia (Authoritative) – Mzazi au mlezi huweka mipaka lakini pia husikiliza maoni ya mtoto na kumwelekeza kwa upendo.
- Malezi ya Kifalme (Authoritarian) – Mzazi au mlezi hutawala kwa amri kali bila kuzingatia maoni ya mtoto.
- Malezi Huria (Permissive) – Mzazi hutoa uhuru mwingi kwa mtoto bila kuweka mipaka ya kutosha.
- Malezi ya Kutelekeza (Neglectful) – Mzazi au mlezi hajishughulishi kabisa na maendeleo ya mtoto.
Umuhimu wa Malezi
- Hujenga msingi wa tabia, maadili, na mwenendo wa mtu.
- Husaidia mtoto kufikia ndoto zake kwa kujifunza kuwajibika na kujitambua.
- Huchangia kupunguza matatizo ya kijamii kama vile uhalifu, matumizi ya dawa za kulevya, na ukosefu wa maadili.
- Huimarisha mahusiano ya kifamilia na kijamii, kwa kuwa mtoto anayelelewa vizuri hujifunza kuheshimu wengine na kushirikiana na watu kwa amani.
- Hutoa mazingira salama kwa ukuaji wa mtoto kimwili na kiakili, kwa kuhakikisha mtoto anapata mahitaji muhimu kama chakula, mavazi, elimu, na afya.
- Hujenga kizazi chenye uwezo wa kuchangia maendeleo ya taifa, kwa sababu malezi bora huandaa watoto kuwa viongozi bora wa baadaye.
- Humwezesha mtoto kuelewa mipaka na nidhamu ya maisha, hivyo kumjengea uwezo wa kufanya maamuzi sahihi.
- Hukuza stadi za maisha kama vile kujiamini, kutatua matatizo, na kushughulikia changamoto kwa njia chanya.
- Huongeza uwezo wa mtoto kupambana na msongo wa mawazo na hali ngumu za maisha, kwa kuwa anakuwa na msingi imara wa kihisia na kiakili.
- Huandaa mtoto kuwa mzazi au mlezi bora wa baadaye, akitumia uzoefu wa malezi aliyopata katika maisha yake.
Wazazi wana jukumu kubwa na la msingi katika maisha ya watoto wao. Wao ndiyo msingi wa malezi bora ambayo huamua mustakabali wa utu wa mtoto katika safari ya maisha yake.
Malezi ya mtoto akiwa tumboni. Katika familia, malezi ya mtoto huanza wakati wa ujauzito wa mama. Malezi ni lazima yazingatie ulaji unaofaa wakati wa mimba na baada ya mtoto kuzaliwa wakati wa kunyonyesha ili kukinga mimba na mtoto mchanga dhidi ya magonjwa. Vitendo wanavyo vifanya wazazi vina mchango mkubwa katika malezi makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kwani mtoto hujifunza kutoka kwao kwa kuona, kusikia na kuiga kile wanachokifanya. Ni muhimu baba na mama kuwasiliana na mtoto aliye tumboni kwa kupapasa tumbo kwa upendo huku wakisema na mtoto maneno yenye heri. Tafiti za kisayansi zinaeleza Kitendo cha mama au baba kumshika au kupapasa tumbo la mimba huku wakiongea, kuimba, au kuwasiliana na mtoto aliye tumboni kuna faida zifuatazo;
Huimarisha Uhusiano wa Kihisia (Bonding) wa mapema kati ya mtoto na wazazi, hata kabla hajazaliwa. Hasa kwa baba, hii ni njia ya kipekee ya kuhusika moja kwa moja na ujauzito na kumtambua mtoto kama sehemu ya familia. Huchochea Ukuaji wa Fahamu za Mtoto (Brain Development). Tafiti za kisayansi zinaonyesha kwamba masikio ya mtotohuanza kufanya kazi kuanzia wiki ya 18–25 za ujauzito, hivyo mtoto anaweza kusikia sauti ya mama au baba. Kuongea na mtoto huchochea ubongo wake kutambua sauti, mdundo, na hisia, hatua muhimu kwa maendeleo ya lugha na hisia. Humtuliza Mtoto Tumboni. Kupapasa kwa upole hutoa hisia za usalama kwa mtoto.
Mtoto anaweza kuguswa au kujibu kwa kutikisa au kujigeuza tumboni, ishara kwamba anahisi na kuitikia. Huimarisha Afya ya Mama Mjamzito. Kitendo hiki huongeza homoni za furaha kama oxytocin kwa mama, ambayo hupunguza msongo wa mawazo, inaboresha usingizi, na kupunguza shinikizo la damu. Mama anapojisikia vizuri, mtoto pia hukua vyema kiafya. Huandaa Mazingira Bora kwa Malezi baada ya Kuzaliwa. Watoto wanaowasiliana kwa sauti na mguso hata kabla ya kuzaliwa, hujenga uhusiano wa karibu zaidi na wazazi baada ya kuzaliwa. Hii pia huchangia utulivu, unyonyeshaji bora, na kujifunza haraka kwa mtoto mchanga.
Malezi baada ya mtoto kuzaliwa. Makuzi (Growth & Maturation): Hii ni hatua za kuaji wa kimwili, kiakili, kihisia na kijamii. Mzazi anapaswa kuzitambua hatua za makuzi ya mtoto katika umri tofauti ili afanye majukumu yake kwa kila hatua ya ukuaji wa mtoto. Ifahamike kuwa, vitendo ama tabia zinazoonekana kwa mtoto wa umri fulani zaweza kutofautiana kidogo na mtoto mwingine wa umri ulele ule. Mtoto anaweza kuwahi ama kuchelewa kufanya vitendo fulani kutegemeana na malezi makuzi na changamshi anaopata toka kwa wazazi/walezi wake.
Ukuaji na tabia zinazoonekana kwa mtoto katika umri 0 hadi miaka 2:
- Mtoto anajifunza kutambua sura za watu, hasa wazazi. Huanza kutambua sauti, kuangalia, na kushika vitu.
- Hujifunza kutambaa, kusimama, na kutembea.
- Huonyesha hisia kama hasira, hofu, furaha au huzuni kwa kulia au kucheka ili kuwasilisha njaa, maumivu au hitaji la upendo
- Huanza kusema maneno machache (mama, baba, maji).
- Hujenga uhusiano wa karibu na mlezi wake (attachment).
- Anaiga tabia rahisi kama kupepea mkono au kucheka.
Wajibu wa Mzazi/Mlezi katika hata hii niKumhudumia mtoto kwa upendo kwa kumshika, kumwimbia na kumlinda. Kumpa mazingira salama ya kucheza na kuchunguza. Kumjibu hisia zake anapolia au anapotaka kujifunza kitu kipya.
Ukuaji na Tabia Zinazoonekana kwa mtoto mwenye umri wa miaka 3 – 4.
- Anajifunza kuongea sentensi rahisi na kuelewa maagizo.
- Huonyesha udadisi mwingi: kuuliza maswali mengi kama “Kwa nini?”
- Anaanza kuonyesha kujitegemea (kupenda kufanya mambo mwenyewe).
- Huanza kucheza na watoto wengine kwa muda mfupi.
- Anaweza kuwa na hasira (tantrums) anaponyimwa kitu.
- Anaanza kuelewa sheria rahisi kama “usiogope” au “subiri”.
Wajibu wa Mzazi/Mlezi: Kumjibu kwa upole na uvumilivu; kutoa maelezo rahisi. Kumpa nafasi ya kujifunza kujitegemea chini ya uangalizi. Kumtuliza kwa huruma na kumweleza namna ya kueleza hisia zake.
Ukuaji na Tabia Zinazoonekana kwa mtoto mwenye umri wa miaka 5–6 (Kujiandaa na kuanza shule).
- Anaiga watu wazima na kutamani kuwa “mwalimu” au “daktari.”
- Anaelewa vizuri lugha na kutumia sentensi ndefu.
- Anaweza kuwa na woga kama wa giza au kuachwa peke yake.
- Anaanza kuelewa tofauti ya kweli na uongo
- Anaanza kujifunza kusoma, kuandika, na kuhesabu
- Anaonyesha woga au kuwa na marafiki wa karibu
- Anaongeza uwezo wa kushirikiana na watoto wengine (cheza kwa makundi).
Wajibu wa Mzazi/Mlezi: Kumfundisha umuhimu wa kushirikiana, kuomba msamaha, na kushukuru. Kumwonyesha mfano bora kwa tabia njema. Kumtia moyo, kumsikiliza, na kumhakikishia kuwa yuko salama.
Ukuaji na Tabia Zinazoonekana kwa mtoto mwenye umri wa miaka Miaka 7–9
- Anaweza kufikiria kwa mantiki na kutatua matatizo rahisi.
- Anakuwa na marafiki wa karibu na anapenda kushindana.
- Hujifunza kufuata sheria na kuelewa maana ya haki na wajibu.
- Anaanza kuwa na hisia za aibu au kujitathmini.
- Anajiamini na kujisikia vibaya kwa kutofanya vizuri.
- Anapenda kushinda.
- Anaonyesha uaminifu kwa rafiki au mtu anayemheshimu.
Wajibu wa Mzazi/Mlezi: Kumpongeza anapojitahidi badala ya kushinda tu. Kumfundisha kushughulikia kushindwa kwa heshima. Kuwa sehemu ya maisha yake ya shule na michezo.
Ukuaji na Tabia Zinazoonekana kwa mtoto mwenye umri wa miaka Miaka 10–12 (kuelekea ya balehe)
- Anaanza kubalehe (hasa wasichana huanza kubadilika kimwili mapema).
- Anaongezeka uwezo wa kujieleza na kujitambua.
- Anapenda uhuru zaidi lakini bado anahitaji uongozi wa karibu.
- Anaweza kuwa na mashaka kuhusu muonekano au uwezo wake.
- Anaanza kujitofautisha na familia, kutafuta utambulisho binafsi.
- Anaweza kuanza kujali sana mitazamo ya wenzake (peer pressure).
- Mabadiliko ya kimwili huanza kuonekana.
- Huwa na hisia kali na hutafuta utambulisho.
- Anapenda uhuru na kushindana na maamuzi ya wazazi.
Wajibu wa Mzazi/Mlezi: Kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa njia sahihi na ya heshima. Kusikiliza maoni ya mtoto na kumshauri kwa staha. Kumjenga katika kujiamini na kuweka mipaka yenye kueleweka.
Ukuaji na Tabia Zinazoonekana kwa mtoto mwenye umri wa miaka Miaka 13–15 (Balehe)
- Hubadilika kimwili (saizi ya mwili, sauti, nywele, hedhi n.k.).
- Anaanza kuchanganyikiwa na hisia: mapenzi, msongo, na wasiwasi.
- Huonyesha uasi au kupinga mamlaka ya wazazi kwa baadhi ya nyakati.
- Anaanza kuwa na mahusiano ya kirafiki ya karibu sana (best friends).
- Huongeza uwezo wa kufikiri kwa undani (abstract thinking).
- Anaweza kushiriki zaidi katika shughuli za kijamii na kujifunza kuwajibika.
Wajibu wa Mzazi/Mlezi: Kudumisha mawasiliano ya wazi, ya kirafiki na yenye kuelewana. Kuweka sheria nyepesi lakini thabiti. Kumwongoza kujua athari za maamuzi (mfano: matumizi ya dawa za kulevya).
Ukuaji na Tabia Zinazoonekana kwa mtoto mwenye umri wa miaka Miaka 16–17 (Ujana wa kati kuelekea utu uzima)
- Anaelekea kuwa huru zaidi kiakili na kijamii.
- Hujitambua zaidi na kuwa na mitazamo ya kipekee
- Huanza kupanga maisha ya baadaye (masomo, kazi, mahusiano).
- Anaweza kuwa na maamuzi ya kina kuhusu imani, maadili, na mahusiano.
- Anatafuta nafasi ya kipekee katika jamii (identity formation).
- Anaelewa zaidi madhara ya tabia (mf. matumizi ya dawa za kulevya, mimba za utotoni).
- Uwezo wa kujitawala huongezeka lakini bado huhitaji ushauri wa watu wazima.
Wajibu wa Mzazi/Mlezi: Kumshirikisha katika maamuzi ya familia au maisha yake. Kumsapoti katika mipango ya baadaye kwa ushauri. Kumpa uhuru wa kuchagua kwa uangalizi na maadili.
Maendeleo ya Mtoto: Kisaikolojia: Mfundishe mtoto kujiamini na kujielewa, mjenge kutambua uwezo na thamani yake, Kijamii: Mfundishe kuheshimu watu wote wakubwa kwa wadogo bila kubagua na bila kuangalia hali zao. Mfundishe namna bora ya kuawasiliana na watu awe mwenye nidhamu na staha, mfundishe kushirikiana na watu katika maswala mbalimbali ya kijamii kwa kutoa msaada wa hali, mali, ushauri utaalamu/ujuzi, tahadhari. Kielimu: Mfundishe kuwa na mshikamano katika maisha ya shule kutumia muda wake kwa kufuata taratibu na miongozo ya shule, kusoma kwa bidii kusaidia wanafunzi wenzake kwa kile anachofanya vizuri zaidi, pia mpe muda wa kujifunza na kupumzika anapokuwa nyumbani. Mpangie ratiba ya kila siku imuongoze anapokuwa nyumbani. Kiroho/kiadili: Kujua mema na mabaya. Mlee mtoto katika njia njema. Awe muumini mzuri wa Kanisani/msikitini ambako atapata malezi endelevu yahusuyo imani yake. Hili litategemea sana mwamko wa wazazi ki imani.
Wajibu wa jumla wa wazazi katika malezi ni pamoja na:
- Kumfundisha na kumpa mtoto mwongozo juu ya maisha, maadili ya kiimani, elimu, tamaduni na maadili ya kijamii; nini wafanye nini wasifanye.
- Kuweka nidhamu ya upendo isiyokuwa ya ukatili.
- Kufuatilia mwenendo na maendeleo ya mtoto kiafya, kielimu, kijamii.
- Kumfundisha mtoto kutambua viashiria vya ukatili anapokuwa nyumbani (fuatilia mazingira anapolala na watu anaolala nao), katika jamii ama shuleni (aina ya marafiki zake na maeneo wanakopendelea kucheza ama kukaa).
- Kuwaeleza watoto hali halisi ya maisha na mabadiliko ki maadili kutokana na mfumo wa utandawazi na mitandao ya kijamii, madhara ya wao kuiga na kufanya mambo yasiyofaa kama kujiingiza kwenye vitendo vya ngono, matumizi ya vileo kama madawa ya kulevya,pombe nk, wizi, matumizi ya lugha za zisizofaa, mavazi na mitindo isiyokuwa ya staha. Mifano mbalimbali ya watu waliokatiza ndoto zao kwa kukaidi kutii maelekezo ya wazazi/walezi wao yaweza kuwasaidia.
- Kuwajengea uwezo katika kutambua thamani yao, kujiamini, na kujisimamia.
- Kumwandaa mtoto anapokaribia bale kwa watoto wa kiume ama kuvunja ungo kwa watoto wa kike ili atambue namna ya kukabiliana na hali za mabadiliko ya mwili.
- Angalizo: Mzazi bora atafanikiwa kumlea mwanae katika misingi bora endapo tu atakuwa mfano halisi kwa kile anachowafundisha na kuwaasa wanae. Kinyume na hapo tunapata watoto wenye tabia tofauti na matarajio kwa kuwa mtu apandacho ndicho avunacho. Tukumbuke kuwa mtoto hujifunza kwa kuona, kusikia na kutenda yale anayoona na kusikia.