ZITAMBUE MBINU NA FAIDA ZA KUSOMA VITABU

By Jamal H. Maherea Kusoma vitabu kuna faida na manufaa mengi kwa mtu binafsi na jamii kwa ujumla.  Kujizoesha kusoma vitabu ni hatua muhimu ya kujenga tabia ya kujifunza na kuboresha ujuzi wa lugha, fikra, na maarifa.  Manufaa haya yanamfanya msomaji kuwa na mtazamo mpana, mwerevu zaidi, na mwenye uwezo bora wa kufikiri kwa makini na kuchanganua masuala. Hizi ni mbinu chache za kujizoesha kusoma vitabu kwa urahisi na ufanisi: 1. Weka malengo madogo ya kusoma. Anza kwa kuweka malengo yanayoweza kufikiwa, kama kusoma kurasa 10 au 20 kwa siku. Malengo haya madogo yatakusaidia kujenga tabia ya kusoma taratibu bila kusikia uzito. Ukiweka malengo makubwa yatakukatisha tama ukishindwa kuyafikia na kupelekea kutokuendelea na usomaji wa vitabu. 2. Chagua vitabu unavyovutiwa navyo   Soma vitabu vinavyokufurahisha au vinavyohusiana na maslahi yako binafsi. Unapoanza na vitabu unavyopenda, kusoma kunakuwa rahisi zaidi na unapata motisha ya kuendelea.  3. Panga muda maalum wa kusoma kila siku na unda mazingira mazuri ya kusoma Weka muda maalum kila siku kwa ajili ya kusoma. Inaweza kuwa asubuhi, mchana, au kabla ya kulala. Kufanya hivi kutakusaidia kujenga utaratibu wa kudumu. Tafuta sehemu tulivu na yenye mwanga mzuri ambapo unaweza kusoma . Ondoa vishawishi kama simu au TV ili uweze kujikita kikamilifu kwenye kitabu. 4. Fanya kusoma sehemu ya ratiba yako  Ongeza muda wa kusoma kwenye ratiba yako ya kila siku kama sehemu ya shughuli zako. Hata kama ni dakika 15 au 30, hiyo inatosha kukuza tabia ya kusoma.  5. Jitunze na thamini maendeleo yako Kila unapomaliza kitabu au kufikia lengo la kusoma, jitunze kwa kitu kidogo kama zawadi au pumziko la kujipongeza. Hii itakupa hamasa ya kuendelea na mpango wako wa kusoma. Kwa kutumia mbinu hizi, utaweza kuunda na kuimarisha tabia ya kusoma vitabu, na polepole utaanza kuona faida kubwa ya maarifa na ustadi unaopata kupitia kusoma. Tuzitambue faida za kusoma vitabu: Kuongeza maarifa:  Vitabu ni vyanzo vikubwa vya elimu. Kusoma vitabu kunakupa taarifa, maarifa, na uelewa wa masuala mbalimbali kama vile historia, sayansi, siasa, na utamaduni. Kuwa na utajiri wa maarifa ni nyenzo muhimu sana ya kukabiliana na changamoto pindi zinapojitokeza maishani mwako. Kufikirisha na kuchochea ubunifu:  Vitabu, hasa vya hadithi au falsafa, vinaweza kuchochea mawazo ya ubunifu na kukuza uwezo wa kufikiri kwa undani na kwa njia tofauti. Kuimarisha umakini na kumbukumbu:  Kusoma vitabu kunahitaji umakini, jambo ambalo linaimarisha uwezo wa kujilenga, kuzingatia, na kuboresha kumbukumbu. Kupunguza msongo wa mawazo:  Kusoma vitabu, hasa vya kuburudisha au vya kujenga fikra, husaidia kupumzisha akili na kupunguza mawazo ya msongo wa maisha ya kila siku. Kuboresha uwezo wa kutatua matatizo: Vitabu vingi vya kihistoria, kisaikolojia, au vya mbinu za maisha vinatoa maarifa kuhusu jinsi ya kutatua changamoto mbalimbali za maisha. Kuwa sehemu ya kikundi cha kusoma vitabu au forum za online: Hii itakupa motisha zaidi, kwani utakuwa na watu wa kubadilishana nao mawazo, na mara nyingi watakusaidia kushikilia utaratibu wa kusoma. Karibu katika website yetu kusoma makala tofauti tofauti zenye faida nyingi na kukujuza mambo mengi yatakayokujenga katika msingi mzuri zaidi na maadili mema.

ZITAMBUE MBINU NA FAIDA ZA KUSOMA VITABU Read Post »

Sifa 10 za mbuni zinazomtofautisha na ndege wengine

By Nasibu Mahinya Ukimshangaa mbuni asiyepaa utamstaajabu ngwini (pengwini); samaki asiyepaa mwenye uwezo wa kuogelea. Kawaida ukimkuta mbuni ndani ya hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro anavyovimba akiwa amejichanganya na pundamilia na nyumbu, wakitafuta malisho unaweza kusahau kuwa huyu ni ndege. Watu wengi wamekuwa wakimuona mbuni kama ndege wa kipekee na wa tofauti basi kama unaisoma hii makala utaweza kuujua utofauti kati ya mbuni na ndege wengine kupitia sifa zake 10. Twenzetu! 1. Muonekano Mbuni ndiyo ndege mrefu, mkubwa na mzito zaidi duniani. Ni mnyama mrefu kuliko wanyama wengine duniani. 2. Mfumo wa mmeng’enyo wa chakula Mbuni ana matumbo matatu na ni ndege pekee ambaye haja zake ndogo na kubwa hutoka tofauti, yani hazichangamani. 3. Mbio na kasi Mbuni anauwezo wa kukimbia kwa kasi ya kilomita 70 kwa saa, kasi kubwa kuliko ndege yoyote yule. Hivyo safari yake ya Dar kwenda Bagamoyo inaweza kumchukua saa moja tu. Hatua yake moja ni sawa na hatua tano za binadamu. Anaweza kuwa na wastani wa kilo 50 kama mbuzi vile lakini pia ana uzito sawa na jumla ya kuku 20. Hii ni ndiyo sababu kuu kwanini mbuni hana uwezo wa kupaa.  Sasa utajiuliza, kwanini kuku ni mwepesi lakini hapai juu angani kama kunguru? Naomba huo uwe mjadala wa siku nyingine. 4. Vidole Mbuni ana vidole viwili tu vya miguuni. Tofauti na ndege wengine wenye vidole vinne ambapo vitatu huangalia mbele na kimoja nyuma, mbuni ana vidole viwili kwenye mguu wake mmoja na vyote vinaangalia mbele. 5. Kujihami Kwenye hatari, silaha kubwa ya mbuni huwa ni mateke yake, hurusha mateke ya mbele yenye uwezo wa kuua wanyama wakali kama fisi, chui hadi simba. 6. Tabia za misimu Katika msimu wa masika mbuni hukaa peke yake ama akiwa na mpenzi wake. Katika msimu wa kiangazi, mbuni hukaa katika makundi ya mbuni wengi hadi 50. Wakati mwingine ndege hao hujichanganya na wanyama wengine kama pundamilia na swala. 7. Mapenzi yao ni ya kipekee Katika kitengo hiki, mbuni ana utaratibu wa kipekee sana. Kwanza jogoo la mbuni hupiga mabawa yake kama anataka kupaa ikiwa ni ishara kwamba anatafuta mwenza.  Akishapata mwenza, wanaanza kutafuta malisho na anahakikisha anampeleka sehemu ambapo hakuna wanyama wengine na wanaendelea kutafuta malisho hapo huku wakizoeana tabia.  Baadaye jogoo la mbuni huanza tena kupiga mabawa kwa nguvu zaidi na kuzunguka akiwa ameyashusha na akiwa anadonoa udongo, ambapo jike la mbuni likishaona hizo ishara basi huchuchumaa na kurusu kupandwa. 8. Yai la mbuni ni bonge la yai Mbuni zaidi ya mmoja huweza kutaga mayai yao kwenye tundu moja na kila mbuni ana uwezo wa kutofautisha mayai yake na ya mbuni wengine.  Yai la mbuni lina uzito wa zaidi ya kilo 1 na ukubwa sawa na nazi. Yai la mbuni bwana, unaweza kulikaangia viazi alimaarufu kwa chipsi mayai sahani kama tano hivi. 9. Jike na dume wote huatamia mayai Jike la mbuni ana rangi ya kijivu na huatamia mayai mchana kwa sababu rangi yake hufanana na mchanga hivyo ni ngumu kuonekana, huku jogoo la mbuni lenye rangi nyeusi hutamia mayai usiku kwa sababu ni ngumu kuonekana gizani. Mayai ya mbuni huchukua siku 35 mpaka 45 kutotolewa. 10. Jicho kubwa sana Jicho la mbuni linalingana na yai la kuku. Jicho la mbuni ni kubwa kuliko ubongo wake. Hivyo ana uwezo mkubwa sana wa kuona mbali na kwenye giza. Mbuni ni mnyama asiyeonekana kirahisi kwa sababu idadi yao imepungua sana hivyo kuwaona ni mpaka mbugani, kwenye hifadhi au kwenye mashamba ya watu binafsi wanapofugwa. Ukitaka kumuona mbuni basi tufunge safari moja kwa moja mpaka kwenye hifadhi za taifa za Serengeti, Mikumi, Ruaha au Katavi. Pia ukitembelea maeneo ya uhifadhi kama Selous na Ngorongoro utaweza pia kujionea mbuni.

Sifa 10 za mbuni zinazomtofautisha na ndege wengine Read Post »

Scroll to Top