By Nasibu Mahinya
- Ni mnyama anayeishi majini na nchi kavu.
- Ana uwezo mkubwa wa kukaa chini ya maji.
Kiboko ni mnyama mla mimea mwenye makazi yake majini na nchi kavu pia.

Wagiriki walimpa jina “Hippopotamus” ikiwa na maana ya farasi wa mtoni.
Kiboko huweka himaya yake majini na shughuli za kuzaliana hufanyika majini , japo jua linapozama hutoka kwenda nchi kavu kwa ajili kula nyasi na huweza kula hadi kilo 70 kwa siku akitembea umbali wa hadi kilomita 10.
Kiboko huishi miaka 40 mpaka 50 na hubeba ujauzito kwa miezi nane.
Kiboko anaweza kuwa na uzito wa kati ya kilo 2,000 hadi elfu 3,700. Mtoto wa kiboko anapozaliwa huwa na uzito wa takribani kilo 45.
Kiboko huonekana kuwa na ngozi nyekundu au zambarau lakini hayo ni mafuta ambayo hutengenezwa na ngozi yake ili kumkinga na jua na wadudu waenezao magonjwa.
Kiboko hajapewa kipawa cha kuogelea lakini kutokana na uwezo wake mkubwa wa kutunza hewa mwilini mwake anaweza kutembea chini ya maji kwa mfano, kwenye sakafu ya mto na hata kupiga hatua kubwa kiasi cha kwamba unaweza kuhisi anaogelea.

Kiboko huzama na kuibuka juu ya maji mara kwa mara takribani kila baada ya dakika tano ili kuvuta pumzi na hii tabia huifanya bila ufahamu wake kiasi cha kwamba hata akiwa amelala anaweza kuifanya bila kuamka.
Kiboko ana uwezo wa kukimbia kwa kasi ya kilomita 30 kwa saa, hivyo safari ya kutoka Dar es Salaam kwenda Bagamoyo inaweza kumchukua takribani saa mbili.
Kiboko na mamba wanaweza kuishi pamoja mtoni lakini kwa mipaka na uangalifu mkubwa, mtoto wa kiboko anaweza kuwa chakula cha mamba au fisi ikiwa wazazi wake hawapo karibu.
Mwaka 2008, Umoja wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Asili (IUCN) umemtaja mnyama kiboko kuwa ni mmoja kati ya wanyama ambao wapo hatarini kupotea kutokana idadi yao kupungua. Nchi ya Demokrasia ya Kongo, kiboko aliwahi kutumika kama kitoweo hadi umoja huo ulipoingilia kati.

Kwa upande wa Tanzania hifadhi za Taifa kama vile, Tarangire, Ruaha, Ziwa Manyara, Serengeti, Mikumi na Katavi zina viboko wengi wa kuvutia. Pia ukitembelea hifadhi ya Taifa ya Nyerere na eneo la hifadhi ya Ngorongoro utaweza pia kujionea viboko wa kukutosha na kujionea kwa macho maisha ya mnyama huyu.